Sep 08, 2021 03:15 UTC
  • Makundi ya mapambano ya Palestina yaitahadharisha Israel

Makundi ya mapambano ya ukombozi wa Palestina yametahadharisha kwamba, hali ya Ukanda wa Gaza inakaribia kuripuka na yameupa utawala wa Israel siku 15 kuruhusu bidhaa muhimu kwa ajili ya raia wa Palestina katika eneo hilo.

Taarifa kali ya makundi hayo iliyowasishwa kwa utawala wa Kizayuni wa Israel kupitia Misri imetahadharisha kuhusu hali mbaya ya eneo la Gaza na kuipa Israel siku 15 kuwa imetekeleza majukumu yake. 

Harakati za mapambano za Palestina zimetangaza katika taarifa hiyo kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel ungali unalizingira eneo la Gaza baada ya vita vya siku 12 na baadaaya usitishaji vita katika eneo hilo.

Harakati hizo zimesisitiza kuwa zinayo machaguo mengi mezani kwa ajili ya kuinyoosha Israel na kukabiliana na siasa zake na kwa sababu hiyo zimeupatia utawala huo fursa yake ya mwisho. 

Taarifa ya harakati za mapambano ya ukombozi wa Palestina imetahadharisha kuwa iwapo Israel itaendeleza siasa za machafuko na kukwepa majukumu yake makundi ya muqawama yatatumia nyenzo zake za mashinikizo. 

Utawala wa Kizayuni wa Israel unalizingira eneo la Ukanda wa Gaza tangu mwaka 2006 wakati Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) ilipoibuka na ushindi katika uchaguzi wa Bunge la Palestina.

Tangu wakati huo Israel imekuwa ikizuia kuingizwa bidhaa zote muhimu katika eneo hilo kama vile chakula, dawa, vifaa vya ujenzi na kadhalika na kulifanya eneo hilo kukabiliwa na hali mbaya. 

Tags