Sep 10, 2021 12:46 UTC
  • Israel yaiomba msaada Jordan kwa ajili ya kuwapata mateka Wapalestina waliotoroka jela

Vyombo vya habari vya Kiebrania vimeripoti kuwa, utawala haramu wa Kizayuni wa Israel umeiomba msaada Jordan kwa ajili ya kuwapata mateka sita Wapalestina waliotoroka jela ya utawala huo ghasibu.

Gazeti la Kiebrania la Israel Hayom limeandika katika toleo lake la leo kuwa, baada ya kupita siku tano tangu mateka sita Wapalestina walipotoroka jela yenye ulinzi mkubwa ya Gilboa kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kugonga mwamba hatua za Wazayuni za kujaribu kuwakamata mateka hao, viongozi wa Tel Aviv wameomba msaada kwa Jordan wa kuwatafuta na kuwakamata Wapalestina hao.

Afisa mmoja wa usalama wa Jordan ameeleza kuhusiana na suala hilo kuwa, Tel Aviv imeitaka nchi hiyo iisaidie kutambua mahali walipo mateka sita Wapalestina endapo watakuwa wamefanikiwa kuvuka mipaka ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Ripoti hii imetolewa leo katika hali ambayo, tovuti ya habari ya Arab48 imenukuu Jumuiya ya Mateka Wapalestina kwamba, utawala haramu wa Kizayuni umewakamata jamaa wengine watano wa familia za mateka Wapalestina.

Wapalestina sita waliotoroka jela ya Israel

Jumatatu wiki hii, mateka sita Wapalestina walifanikiwa kutoroka jela yenye ulinzi wa hali ya juu kabisa ya Gilboa kaskazini ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu kwa kuchimba mashimo na kutengeza njia ya chini ya ardhi.

Mara baada ya kupata taarifa ya kutoroka Wapalestina hao, vikosi vya usalama vya utawala haramu wa Israel vilianzisha operesheni ya msako katika maeneo mbalimbali sambamba na kushadidisha vitendo vya ukatili dhidi ya mateka wengine Wapalestina wanaoshikiliwa katika jela za utawala huo na kuwatia nguvuni pia jamaa kadhaa wa familia za Wapalestina hao sita.../

Tags