Sep 10, 2021 12:50 UTC
  • Januari 31 yatangazwa kuwa siku ya mwisho ya askari wa Marekani kuwepo katika ardhi ya Iraq

Kamandi Kuu ya operesheni za pamoja za jeshi la Iraq imetangaza tarehe ya mwisho kwa askari wa jeshi la Marekani kuwepo katika ardhi ya nchi hiyo.

Tahsin al-Khafaji, msemaji wa Kamandi Kuu ya operesheni za pamoja za jeshi la Iraq ameeleza leo kuwa kwa mujibu wa matokeo ya mazungumzo ya kistratejia yaliyofanywa baina ya nchi mbili, kamati ya pamoja ya Iraq na Marekani imetangaza kuwa, Januari 31 2022, ndio siku ya mwisho kwa askari wa jeshi la Marekani kuwepo katika ardhi ya Iraq.

Al-Khafaji ameongeza kuwa, kufuatia makubaliano hayo, askari wengi wa jeshi la Marekani wameanza kuondoka nchini Iraq.

Msemaji wa Kamandi Kuu ya operesheni za pamoja za jeshi la Iraq amebainisha pia kwamba, Wamarekani hawana kambi au vituo vya kijeshi nchini humo isipokuwa sehemu ndogo tu waliyotengewa katika kituo cha anga cha Ainul-Asad, ambacho hivi sasa kinaendeshwa na jeshi la Iraq; na vile vile wametengewa sehemu ndogo tu ya kituo cha al Hariri, ambacho sehemu yake kubwa inadhibitiwa na vikosi vya Peshmerga vya eneo la Kurdistan ya Iraq.

Askari vamizi wa Marekani wakiranda katika mitaa ya Iraq

Katika safari aliyofanya hivi karibuni nchini Marekani na katika mazungumzo juu ya masuala mbalimbali aliyofanya na Rais wa nchi hiyo Joe Biden, Waziri Mkuu wa Iraq Mustafa al-Kadhimi alisisitizia ulazima wa kuhakikisha ifikapo tarehe 31 Desemba 2021, askari wa Marekani wawe wameshaondoka nchini Iraq.

Askari wa jeshi vamizi la Marekani wamepiga kambi nchini Iraq tangu mwaka 2003, ilhali wananchi, makundi na mirengoi mbalimbali ya Iraq wanataka askari hao waondoke nchini humo. Bunge la Iraq pia limepitisha mpango unaotaka askari wa Marekani waondoke katika ardhi ya nchi hiyo.../

Tags