Sep 15, 2021 10:18 UTC
  • Nukta kadhaa za kuzingatia kuhusu madai ya Imarati ya kupambana na ugaidi

Umoja wa Falme za Kiarabu, Imarati, umeongeza majina ya watu 38 na mashirika 15 katika orodha yake ya watu wanaodaiwa kuunga mkono ugaidi ambapo majina ya Wairani kadhaa yanaonekana katika orodha hiyo.

Hatua hiyo ya Imarati inapasa kuchunguzwa katika pande kadhaa.

Nukta ya kwanza ni kuwa watu waliowekwa kwenye orodha hiyo ni raia kutoka nchi za Imarati, Lebanon, Iraq, India, Yemen, Afghanistan, Syria, Nigeria na Iran. Mashirika yaliyowekwa kwenye orodha hiyo pia yanajishughulisha na masuala ya biashara, ubaharia na ubadilishaji wa fedha za kigeni. Kwa msingi huo mashirika na watu waliowekwa katika orodha hiyo inayodaiwa kuwa ya magaidi wanajishughulisha na masuala ya uchumi. Kabla ya hapo pia Imarati iliweka katika orodha hiyo na kwa nyakati tofauti majina ya watu wengine waliodaiwa kuwa ni magaidi wakiwemo raia wa Iran.

Nukta ya pili ni kwamba, serikali ya Imarati inadai kuwa umechukua hatua hiyo kwa ajili ya kulenga na kusimamisha shughuli za mitandao inayodhamini kifedha vitendo vya ugaidi. Hatua hiyo imechukuliwa katika hali ambayo serikali ya Abu Dhabu haijatoa nyaraka wala ushahidi wowote wa kuthibitisha madai hayo. Madai ya uungaji mkono ugaidi hutolewa mara kwa mara na pande tofauti bila kutolewa maana halisi ya neno ugaidi wala kuarifishwa watu wanaoudhamini kifedha au vinginevyo.

Kinyume na madai ya Imarati, watawala wa nchi hiyo wanashirikiana kwa karibu na Wazayuni ambao wanatekeleza jinai za kutisha dhidi ya Wapalestina

Ni kutokana na hali hiyo ya kutojulikana au kutoarifishwa vyema suala hilo ndipo Imarati ikalituhumu huko nyuma kundi la Ikhwanul Muslimeen ambalo lina wafuasi wengi katika ulimwengu wa Kiarabu kuwa ni kundi la kigaidi na hivyo kuamua kuwatia nguvuni viongozi wake. Mbali na hayo, Imarati pia imeyatia makundi mengine kadhaa ya mapambano ya Kiislamu katika eneo katika orodha hiyo bandia ya ugaidi.

Nukta ya tatu ni kuwa Imarati inadai kupambana na ugaidi katika hali ambayo yenyewe imekuwa ikishirikiana kwa miaka mingi na makundi mashuhuri ya ugaidi duniani. Rais Joe Biden wa Marekani ambaye kabla ya hapo alikuwa Makamu wa Rais Barack Obama alizituhumu Saudi Arabia na Imarati kuwa waungaji mkono wakuu wa ugaidi katika Masharikiya Kati kutokana na uungaji mkono na masaada wao mkubwa wa mamia ya mamilioni ya dola kwa makundi ya kigaidi na hasa al-Qaida, Jabhat an-Nasra na makundi mengine ya kitakfiri yaliyokuwa yakipigana kwa ajili ya kuangusha serikali halali ya Rais Bashar al-Asad wa Syria.

Kwa hakika katika muongo mmoja uliopita, Imarati imekuwa moja ya nchi muhimu zinazounga mkono makundi ya kigaidi na kitakfiri katika eneo na hasa nchini Syria ambapo imekuwa ikitoa msaada mkubwa wa kifedha kwa makundi hayo kwa lengo la kuiangusha serikali halali iliyochaguliwa na watu wa nchi hiyo. Kwa msingi huo ni kichekesho kikubwa kuona kuwa nchi hiyo ya kifalme ambayo inajulikana kwa kuunga mkono makundi ya kigaidi imejitokeza na kubuni orodha bandia eti ya watu na mashirika yanayounga mkono ugaidi.

Nukta ya nne ni kwamba Imarati inadai kupambana na ugaidi katika hali ambayo yenyewe ina rekodi ndefu na chafu ya ukiukaji wa haki za binadamu. Wanaharakati wengi wa kisiasa na kiraia wamekamatwa na kupewa mateso makali na serikali ya nchi hiyo kutokana na tuhuma mbalimbali zisizo na msingi za eti kuunga mkono ugaidi. Ahmad Mansur ambaye ni muhandisi wa umeme raia wa nchi hiyo ni mmoja wa watu wanaopata mateso hayo makali wakiwa kifungoni. Alitiwa nguvuni mwaka 2017 kwa tuhuma za kuivunjia heshima serikali ya Imarati  na karibuni aliandika kwamba anapata mateso makali ya kimwili na kiroho kwenye jela.

Imarati ni miongoni mwa wakiukaji wakubwa wa haki za binadamu

Mwanaharakati huyo anayetetea haki za kiraia, anapata mateso hayo kwenye jela katika hali ambayo hana kosa lolote isipokuwa kutaka marekebisho ya kisiasa yafanyike nchini.

Kwa msingi huo ni kichekesho kuona kuwa nchi ambayo ni miongoni mwa nchi kuu zinazokiuka wazi haki za binadamu za raia wake imeamua kubuni orodha bandia ya ugaidi na kuweka humo majina ya watu na mashirika yanayodaiwa kuunga mkono ugaidi bila ya kutoa ushahidi wowote wa maana katika uwanja huo.

Mbali na hayo, Imarati wakati huo huo inashirikiana na makundi ya kigaidi na tawala ambazo ni mashuhuri kwa kukiuka haki za raia wake na kuunga mkono uagaidi katika eneo yaani utawala haramu wa Israel na Saudi Arabia, katika kuwakandamiza watu wa Yemen wasio na hatia yoyote.

Tags