Sep 16, 2021 12:17 UTC
  • Waziri wa Lebanon: Mafuta ya Iran yamevunja vikwazo vya kidhalimu vya Marekani

Waziri wa Kazi wa serikali mpya ya Lebanon amesema sambamba na kuingia misafara ya mafuta ya Iran katika ardhi ya nchi hiyo kwamba, shehena hizo za mafuta zimevunja mzingiro wa kihistoria na wa kidhalimu ambao Marekani ilikuwa imeiwekea Lebanon.

Televisheni ya al Manar imemnukuu Muṣṭafá Bayram akisema hayo leo Alkhamisi na kusisitiza kuwa, kwa kuingia misafara ya mafuta ya Iran katika ardhi ya Lebanon, nchi hiyo imeweza kuvunja vikwazo na mzingiro wa kihistoria na wa kidhalimu uliokuwa umewekwa na Marekani na baadhi ya nchi.

Naye Gebran Bassil, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Lebanon ambaye ni mkuu wa chama cha Mrengo wa Kitaifa wa Ukombozi wa Lebanon amesema kuhusu kuingia misafara ya mafuta ya Iran kutokea Syria kwamba wakati maadui wa taifa na wananchi wa Lebanon walipofanya njama za kuwatesa wananchi hao kwa kuwanyima mafuta, wananchi hao wana haki ya kudhamini mahitaji yao ya bidhaa hiyo muhimu kutoka sehemu yoyote ile.

Gebran Bassi, Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani wa Lebanon

 

Vyombo vya habari vya Lebanon, leo asubuhi vimetangaza habari ya kuingia katika ardhi ya Lebanon, msafara wa kwanza wa mafuta ya Iran ukiwa na malori 20 ya kubebea mafuta.

Televisheni ya al Manar imesema kuwa, msafara huo utakwenda katika mji wa Baalabak na kumimina mafuta yake huko. 

Muda mchache baada ya msafara wa kwanza kuingia katika ardhi ya Lebanon, misafara mingine mitatu yenye malori ya mafuta ya Iran nayo imeingia katika ardhi ya nchi hiyo.

Jumapili wiki hii, meli ya mafuta ya Iran ilitia nanga katika bandari ya Baniyas nchini Syria na misafara minne ya malori ya mafuta hayo imeingia katika ardhi ya Lebanon leo Alkhamisi.

Tags