Sep 17, 2021 08:05 UTC
  • Hali ya hatari kusini mwa Yemen; kufeli kikamilifu muungano vamizi wa Kisaudi

Aidarus al Zoubaidi, mkuu wa baraza lijiitalo "Baraza la Mpito la Yemen" ambalo ni la mamluki wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) ametangaza hali ya hatari na kutotoka nje katika mikoa ya kusini mwa Yemen. Hali hiyo ya hatari imetangazwa baada ya wananchi wa miji tofauti ya kusini mwa nchi hiyo kufanya maandamano makubwa ya kulalamikia wavamizi na mamluki wao.

Maandamano ya wananchi wa kusini mwa Yemen yanaendelea kwa mwezi mzima sasa. Mikoa ya Aden, Taiz, Hadhramout, al Mahra na Lahij ndiyo iliyokumbwa na maandamano makubwa zaidi ya wananchi. Sababu kuu ya maandamano hayo ni kulalamikia hali mbali ya kimaisha na kijamii katika mikoa hiyo ya kusini mwa Yemen. Kumezuka pia mapigano ya silaha baina ya mamluki wa Saudia na Imarati, na hiyo imetajwa kuwa ni moja ya sababu zilizompelekea mkuu wa baraza la mpito la kusini kutangaza hali ya hatari na marufuku ya kutotoka nje katika mikoa yote ya kusini mwa Yemen.

Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) ni moja ya wavamizi wakuu wa nchi ya Kiislamu ya Yemen. Baraza hilo la mamluki wa Imarati liliundwa mwaka 2017 na hivi sasa linadhibiti mkoa wa Aden. Linadhibiti pia mkoa wa Socotra wa kusini mashariki mwa Yemen na baadhi ya maeneo mengine ya kusini mwa nchi hiyo. 

Moja ya sababu za hasira za wananchi wa kusini mwa Yemen ni kushindwa mamluki wa Saudia na Imarati katika medani za vita

Kwa mwezi mzima sasa wananchi wamekuwa wakifanya maandamano kushinikiza kupinduliwa mamluki wa Saudia na Imarati huko kusini mwa Yemen. Hata hivyo mamluki hao wamekuwa wakitumia nguvu kupita kiasi kukandamiza maandamano ya wananchi hao ambapo habari ya karibuni inasema kuwa mtu mmoja ameuliwa kwa kupigwa risasi na mamluki hao na wengine kadhaa wamejeruhiwa. Harakati moja ya wananchi wa Yemen imesema, Saudi Arabia ndiyo inayoongoza ukandamizaji huo. Harakati ya "Shabab Adan al Thair" yaani vijana wanamapinduzi wa Yemen imesema kuwa amri ya kukandamizwa wananchi wa kusini mwa Yemen imetolewa moja kwa moja na Saudi Arabia ambayo ni adui mkubwa wa taifa la Yemen.

Mbali na ugumu wa maisha, wananchi wa mikoa ya kusini mwa Yemen wanalalamikia pia kuporomoka thamani ya safaru ya taifa, kuzimwa muda mrefu umeme na huduma sifuri zinazotolewa na wanaoshikilia mikoa hiyo. 

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, sababu kuu ya hali mbaya kama hiyo kwenye mikoa ya kusini mwa Yemen ni kuweko tawala mbili zinazokinzana, moja ni utawala wa mamluki wa Imarati na mwingine ni wa mamluki wa Saudi Arabia. Hata hivi sasa kuna serikali mbili kusini mwa Yemen moja ni ya Mansour Hadi, rais aliyejiuzulu na kukimbilia Saudi Arabia na nyingine ni ya Aidarus al Zoubaidi, mkuu wa baraza lijiitalo la mpito la Yemen ambalo ni la mamluki wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati). Gazeti la al Quds al Arabi limeandika: Kauli mbiu kuu ya waandamanaji wa kusini mwa Yemen ni kutoka nchini humo serikali za Mansour Hadi na Aidarus al Zoubaidi. 

Sababu nyingine inayokwamisha mambo huko kusini mwa Yemen ni kuweko mikono mingi ya wageni ambao kila mmoja anafikiria maslahi yake binafsi bila ya kujali kabisa matakwa na maslahi ya wananchi wa mikoa hiyo. Mbali na Saudia na Imarati, madola ya kibeberu kama utawala wa Kizayuni wa Israel, Uingereza na Marekani yamejikita sana katika mikoa ya kuisni mwa Yemen hasa katika maeneo nyeti na muhimu ya kiuchumi na kiusalama. Waandamanaji wa Yemen wanasikika wakilaani uvamizi wa madola hayo na kutaka ukombozi wa ardhi zao kutoka kwenye makucha ya mabeberu hao wasiojali chochote isipokuwa maslahi yao binafsi. 

Wananchi wa kusini mwa Yemen wamekasirishwa pia na kushindwa wavamizi kulinda usalama wao na vita baina ya wavamizi wenyewe kwa wenyewe

 

Sababu nyingine ya kushuhudiwa maandamano makubwa ya wananchi huko kusini mwa Yemen, ni kushindwa muungano vamizi wa Kisaudi katika medani za vita. Muungano huo vamizi si tu umeshindwa kumrejesha madarakani Mansour Hadi mjini San'a, lakini pia umeshindwa kuwadhaminia usalama na utulivu wananchi wa mikoa ya kusini inayodhibitiwa na mamluki wao. 

Naam kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya kisiasa, hasira kubwa za wananchi wa mikoa ya kusini mwa Yemen imetokana na kipigo kikali walichopata wavamizi wa Yemen katika medani za vita na kushindwa kutimiza ahadi walizotoa. Inaonekana wazi kwamba wimbi la maandamano ya wananchi wa mikoa ya kusini mwa Yemen ambalo limetokana na kuchoshwa wananchi hao na wavamizi wa nchi yao ni ushahidi wa wazi wa kufeli kikamilifu muungano vamizi wa Saudia-Imarati nchini Yemen.