Sep 17, 2021 11:23 UTC
  • Wananchi wa Argentina waandamana kuliunga mkono taifa la Palestina

Wanaharakati wa kisiasa na viongozi wa asasi za kijamii na za haki za binadamu nchini Argentina wameandamana wakitangaza himaya na uungaji mkono wao kwa wananchi madhulumu wa Palestina.

Waandamanaji hao wakiwa wamebeba mabango na maberamu wamepaza sauti wakilaani jinai za utawala haramu wa Israel na kusisitiza kuwaunga mkono wananchi wa Palestina na kueleza kwamba, muqawama na mapambano ya wananchi wa Palestina ni halali kwa ajili ya kukabiliana na utawala vamizi wa Israel.

Maandamano hayo yaliyofanyika katika mji mkuu wa Argentina Buenos Aires yaliishia katika medani inayoolekea katika ikulu ya Rais.

Roberto Cirilo Perdia, mmoja wa makamanda wa mapambano dhidi ya udikteta nchini Argentina katika muongo wa 70 alikuwa mmoja wa watu waliohutubia katika hadhara ya waandamanaji hao.

Akihutubia katika mkusanyiko huo Roberto Cirilo Perdia amesema, Wazayuni wanadhani kwamba, kwa kufanya jinai na kwa kupita zama, mapambano halali ya wananchi wa Palestina yatafifia na kuzimika na hivyo kusambaratika.

Bendera ya Palestina

 

Aidha amesema, hii leo baada ya kupita miaka 70 tangu kuanzishwa utawala wa kibaguzi wa Israel, mapambano na muqawama wa Palestina ungali hai na uko imara zaidi kuliko wakati mwingine wowote ule.

Carlos Aznares, mwanahabari mashuhuri na mwanaharakati wa haki za binadamu nchini Argentina ni miongoni mwa wanaharakati wengine waliohutubia katika maandamano hayo ambapo alisoma pia tangazo la waandamanaji la kufungamana na wananchi wa Palestina pamoja na azimio lililotiwa saini na makumi ya asasi za haki za binadamu nchini Argentina ambalo linalaani vitendo na jinai za utawala haramu wa Israel huko Palestina.

Tags