Sep 19, 2021 02:24 UTC
  • Muqawama wa Palestina wakataa mpango wa Israel wa

Muqawama wa Palestina umesisitizia ulazima wa kuendelea kutoa mashinikizo kwa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na kueleza kwamba hautaruhusu wala kukubali mpango wa Kizayuni wa "Uchumi Mkabala wa Usalama".

Afisa mmoja katika Kamandi ya makundi ya muqawama ya Palestina amesisitiza kuwa, mpango wa waziri wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni Yair Lapid uitwao "Uchumi Mkabala wa Usalama", hauna umuhimu wowote kwa makundi hayo.

Afisa huyo wa muqawama wa Palestina amebainisha kuwa, lengo la mpango huo ni kuyapokonya silaha makundi ya muqawama au kuyafungamanisha masuala ya kitaifa na misingi ya kadhia ya Palestina na baadhi ya masuala ya kiuchumi.

Kwa mujibu wa afisa huyo, muqawama wenyewe utazirejesha haki za taifa la Palestina, tena kwa mbinu zile zile ulizozizoea na kwa namna itakayoulazimisha utawala wa Kizayuni ukubali masharti yake.

Ameeleza kwamba kwa sasa, na kutokana na mashinikizo ya makundi ya muqawama, utawala haramu wa Kizayuni umelazimika kuwasahilishia mambo Wapalestina, kuachana na hatua ulizokuwa ukichukua huko nyuma na kutekeleza kile unachotaka muqawama.

Ameashiria pia jitihada za makundi ya muqawama za kufanikisha kwa namna ya kuheshimika ubadilishanaji wa mateka Wapalestina na akasema, makundi hayo hayataruhusu utawala wa Kizayuni au kundi jengine lolote lile litekeleze mpango linaoutaka, kwani utafeli kama ilivyotokea huko nyuma.

Waziri wa mambo ya nje wa utawala haramu wa Israel Yair Lapid, siku ya Jumapili iliyopita alitangaza uamuzi wa kulegeza msimamo na kuachana na chaguo la nguvu za kijeshi na badala yake akazungumzia mpango mpana alioutaja kuwa ni wa kuishinda harakati ya HAMAS katika Ukanda wa Gaza kwa kutumia mbinu za kiuchumi na kidiplomasia.../

Tags