Sep 20, 2021 02:29 UTC
  • Waziri wa Masuala ya Kidini wa Israel: Katu hatutaruhusu kuundwa nchi ya Palestina

Waziri wa Masuala ya Kidini wa utawala haramu wa Israel amesema kuwa, serikali ya sasa ya utawala huo, haitaruhusu kwa namna yoyote ile kuundwa nchi ya Palestina.

Matan Kahana, Waziri wa Masuala ya Kidini wa utawala wa Kizayuni wa Israel amekariri sera za utawala huo ghasibu za kuzuia kuundwa nchi huru ya Palestina mji mkuu wake ukiwa Baitul-Muqaddas.

Aidha amesema kuwa, serikali ya Waziri Mkuu wa Israel Naftali Bennett katu haitachukua mkondo au mwenendo wa kisiasa utakaopelekea kuundwa dola huru la Palestina.

Mwezi uliopita, Naftali Bennett Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel alitangaza wazi kuwa, anapinga vikali kuundwa nchi ya Palestina na kwamba, hayuko tayari hata kukaa meza moja na Mamlaka ya Ndani ya Palestina kwa ajili ya kujadili suala hilo. 

Kadhalika Naftali Bennett alisisitiza kwamba, serikali ya utawala wa Kizayuni wa Israel chini ya uongozi wake itasukuma mbele gurudumu la kutekeleza mipango ya ujenzi wa vitongoji zaidi vya walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Hayo yanajiri huku Mamlaka ya Ndani ya Palestina  ikiendelea kuitaka jamii ya kimataifa ichukue hatua za maana na za kivitendo ili kuzuia hatua za upande mmoja na zilizo kinyume cha sheria za utawala haramu wa Israel za kupanua vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.

Utawala huo ulizikaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina katika vita vya mwaka 1967;  na azimio la Geneva linasema kuwa ni marufuku utawala wa Kizayuni kufanya shughuli zozote za ujenzi katika ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu.