Sep 20, 2021 12:48 UTC
  • Onyo kali la Meja Jenerali Mohammad Bagheri kwa makundi ya kigaidi na waungaji mkono wao

Katika miaka ya karibuni, makundi ya kigaidi na kwa uungaji mkono wa Marekani na utawala haramu wa Israel yameongeza ugaidi na mashinikizo ya juu ya kiusalama dhidi ya Iran katika maeneo ya mpakani na ndani ya mipaka ya Iran.

Hata kama harakati za kigaidi za makundi hayo zimekuwa zikijibiwa kwa wakati na Iran, lakini matamshi yaliyotolewa Jumapili na Meja Jenerali Mohammad Bagheri, Kamanda Mkuu wa Kamandi Kuu ya Majeshi ya Iran yanachukuliwa kuwa onyo kali kwa makundi hayo.

Mohammad Bagheri amesema: Kwa bahati mbaya eneo la kaksazini mwa Iraq linakabiliwa na matatizo kutokana na udhaifu wa serikali ya ndani ya eneo hilo na vilevile ya serikali kuu ya Iraq kutokana na uwepo wa Wamarekani, jambo ambalo limeyapelekea makundi yaliyo dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kuimarisha harakati zao za kigaidi katika eneo hilo.

Meja Jenerali Mohammad Bagheri amesisitiza kwamba jeshi la Iran likiongozwa na Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu Sepah, litayatokomeza makundi hayo na kwamba operesheni zilizoanza dhidi ya makundi hayo wiki mbili zilizopita zitaendelea, kwa sababu ni haki ya kimsingi ya taifa la Iran kulinda mipaka yake na kudumisha amani na utulivu katika mipaka hiyo.

Kuna nukta mbili za kuzingatia kuhusu suala hili.

Shambulio dhidi ya kituo cha utawala wa Israel katika eneo la Arbil kinachotumika kufanya ujasusi dhidi ya Iran

Ya kwanza ni kuwa baada ya Marekani kuivamia kijeshi Iraq, nchi hiyo ya Kiarabu imegeuka na kuwa kituo muhimu cha magaidi ambacho kinatumiwa na Marekani kuhatarisha usalama wa Iran.

Nukta ya pili ni kwamba ni haki ya kila nchi kujibu na kukabiliana na makundi ya kichokozi na kigaidi ambayo yanahatarisha usalama wa mipaka yake.

Katika uwanja huo Meja Jenerali Mohammad Bagheri ametaja kambi ya Harir ya Marekani nchini Iraq kuwa moja ya vituo vinavyotumika kuhatarisha usalama wa Iran na kusema: Hatutavumilia kuona kambi hiyo ikiwa karibu na mipaka yetu na kutumika kama kituo cha vikao vya kupanga njama dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu. Wanapasa kuvunja kambi hiyo na tayari kazi imeanza na itaendelea kwa nguvu zote. Shughuli za kidiplomasia na kijeshi zinapasa kutekelezwa kwa ajili ya kuimarisha usalama na utulivu wa kudumu katika eneo.

Bila shaka Iran itachukua hatua madhubuti na za haraka katika uwanja huo. Baada ya Marekani kutekeleza jinai ya kumuua kigaidi Luteni Jenerali Haj Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Kamanda wa Kikosi cha Kujitolea cha Wananchi wa Iraq (Hashd al Shaabi) karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad tarehe 3 Januari 2020, jeshi hilo la walinzi wa Mapinduzi lilivurumisha makombora ya kulipiza kisasi katika kambi muhimu na kubwa zaidi ya jeshi la Marekani ya Ain al-Asad huko Iraq. Shambulizi hilo la kulipiza kisasi liliharibu sehemu kubwa ya kambi hiyo ambayo ilikuwa ikitumika kama kituo cha kupanga njama za kigaidi dhidi ya Iran.

Marekani imeongeza uwepo wake wa kijeshi katika Asia ya Magharibi kwa kisingizio cha kuimarisha uthabiti na usalama lakini kinyume na madai hayo kila mara inapoongeza uwepo huo, makundi ya kigaidi huongezeka na hivyo kuhatarisha zaidi usalama wa eneo. Baada ya kuikalia Iraq kwa mabavu Marekani ilijenga vituo vya kijeshi katika mikoa ya Baghdad, al-Anbar, Dahouk, Arbil, Kirkuk, Nainawa na Swalah ad-Deen mbali na kuanzisha vituo vingine vya siri na vya mafunzo ya kijeshi katika miko mingine ya nchi hiyo.

Kituo cha kijeshi cha Marekani cha Ain al-Asad nchini Iraq

Mujtaba Shahsuni, mtaalamu wa masuala ya kimataifa anasema kuwa Marekani imekuwa na nafasi kubwa hasi katika kuvuruga utulivu wa Asia Magharibi. Anasema: Marekani ina vituo vingi vya kijeshi, vya wazi na vya siri katika eneo ambapo ilitoa visingizio mbalimbali vikiwemo vya eti kuimarisha usalama ili kuhalalisha ujenzi wake. Lakini historia imethibitisha kuwa uwepo mkubwa wa kijeshi wa Marekani katika eneo haujasaidia lolote isipokuwa kuvuruga usalama na utulivu wa eneo hili muhimu kistratijia.

Ni wazi kuwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa serikali kuu ya Iraq na ya utawala wa ndani katika eneo la Kurdistan zina jukumu muhimu la kulinda usalama katika mipaka yao na kutoruhusu kutumiwa na makundi ya kigaidi na askari wa kigeni katika kuhatarisha usalama wa nchi jirani. Kwa msingi huo serikal hizo zinalazimika kuvunja vituo vyote vya magaidi katika ardhi yao ili kuzuia mashambulio na njama za kigaidi dhidi ya taifa la Iran.