Sep 21, 2021 03:44 UTC
  • Bunge la Lebanon laipigia kura ya kuwa na imani nayo serikali ya Waziri Mkuu Mikati

Bunge la Lebanon limeipigia kura ya kuwa na imani nayo serikali ya Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo Najib Mikati.

Baada ya mchakato wa upigaji kura uliofanyika jana usiku, Spika wa bunge Nabih Berri alitangaza kuwa, serikali ya Mikati imefanikiwa kupata wingi wa kura za uungaji mkono wa bunge kwa kupitishwa kwa kura 85 katika kikao kilichohudhuriwa na wabunge 100.

Wabunge 15 waliamua kutoipigia kura serikali mpya ya Lebanon itakayoongozwa na Mikati.

Najib Mikati alikabidhiwa jukumu la kuunda serikali na Raia Michel Aoun mnamo tarehe 26 Julai.

Tangu mwezi Agosti mwaka jana hadi sasa, Lebanon imekuwa ikiendeshwa bila ya kuwa na baraza rasmi la mawaziri; na Hassan Diab amekuwa akihudumu kama waziri mkuu wa serikali ya mshikizo tu.

Rais Michel Aoun wa Lebanon

Baada ya kutokea mripuko katika bandari ya Beirut Agosti 4 mwaka uliopita wa 2020 na kujiuzulu waziri mkuu Diab, kiongozi wa harakati ya Al Mustaqbal Saad Hariri alipewa jukumu la kuunda serikali, lakini kutokana na kutoa visingizio mbalimbali na kwa sababu ya kutofautiana na Rais Michel Aoun juu ya baadhi ya mambo, baada ya kupita miezi tisa hakuweza kutekeleza jukumu hilo; na hatimaye mnamo tarehe 15 Julai mwaka huu akatangaza uamuzi wa kughairi kukamilisha jukumu hilo.../