Sep 21, 2021 12:37 UTC
  • Mamilioni ya Wayemen waandamana kuadhimisha Mapinduzi ya nchi hiyo

Mamilioni ya wananchi wa Yemen leo Jumanne wamefanya maandamano makubwa katika mkoa wa Saada wa kaskazini wa nchi hiyo kwa mnasaba wa maadhimisho ya tarehe 21 Septemba, siku ya mapinduzi ya nchi hiyo.

Televisheni ya al Masirah imetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, waandamanaji wamebeba picha za Abdul Malik Badruddin al Houthi, Kiongozi Mkuu wa harakati ya Ansarullah ya Yemen ili kuadhimisha mapinduzi ya wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu.

Mwaka 2014 katika siku kama ya leo, wananchi wa Yemen walifanya mapinduzi yaliyoing'oa madarakani serikali ya vibaraka wa Saudi Arabia.

Tangu mwaka huo hadi hivi sasa wananchi wa Yemen wanaadhimisha siku hiyo kila mwaka kwa jina la siku ya ukombozi.

Abdul Malik Badruddin al Houthi

 

Mwezi Machi 2015, Saudi Arabia ilianzisha mashambulizi makubwa ya kivamizi dhidi ya wananchi wa Yemen kwa uungaji mkono kamili wa Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel, madola mengine ya kibeberu ya Marekani na kwa ushirikiano mkubwa na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na baadhi ya nchi za Kiarabu kama Sudan.

Tangu wakati huo hadi hivi sasa madola hayo vamizi yameizingira kila upande Yemen kutokea angani, baharini na ardhini na hawaruhusu chochote kuingia wala kutoka nchini humo. Hiyo ni jinai nyingine kubwa inayofanywa na wavamizi wa nchi ya Kiislamu ya Yemen.

Hadi hivi sasa uvamizi huo wa Saudia na kundi lake umeshasababisha zaidi ya Wayemen 17,000 kuuawa, makumi ya maelfu wengine kujeruhiwa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.