Sep 22, 2021 12:51 UTC
  • Jihadul-Islami ya Palestina: Kipaumbele kwa sasa ni kukabiliana na Wazayuni maghasibu

Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina imesisitiza kuwa kipaumbele cha Wapalestina kwa sasa ni kukabiliana na Wazayuni maghasibu.

Taarifa iliyotolewa leo na harakati hiyo ya muqawama ya Palestina imesema: "Sisi tunatangaza kwa mara nyingine tena kuwa tunapinga kufanyika uchaguzi wa ndani, bila kukubaliana kwanza juu ya mpango utakaobainisha wazi kuhusu kukabiliana na maghasibu."

Katika sehemu nyingine ya taarifa yake hiyo, Jihadul-Islami imesisitiza kuwa, kuitisha uchaguzi wowote ule katika mazingira ya uvamizi na kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina ni sawa na kujaribu kukwepa mkakati wa kitaifa kuhusu namna ya kupambana na adui. Taarifa hiyo imeongezea kwa kusema: "Hali ya sasa inahitaji pande zote kujikita katika kupanga namna ya kukabiliana na maghasibu na mashambulio ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.

Hivi karibuni, Mamlaka ya Ndani ya Palestina ilitoa agizo la kuitishwa katika awamu mbili chaguzi za vijiji na vitongoji vya Palestina tarehe 11 Desemba mwaka huu.

Uchaguzi wa mwishi wa vitongoji na vijiji huko Palestina ulifanyika miaka ya 2017-2018, ambapo harakati ya Fat-h ilishinda kwa kura nyingi huku harakati ya Hamas ikisusia uchaguzi huo na kutoruhusu ufanyike pia katika Ukanda wa Gaza.

Kwa mujibu wa kanuni na sheria za Palestina chaguzi hizo inapasa zifanyike kila baada ya miaka minne.

Wakati huohuo Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Muhammad Shtayyeh ameitaka harakati ya Hamas iruhusu kufanyika awamu ya kwanza ya chaguzi hizo za vitongoji na vijiji katika Ukanda wa Gaza.../