Sep 23, 2021 11:42 UTC
  • Sababu za Wapalestina kutaka Mahmoud Abbas atoke madarakani

Katika hali ambayo Wapalestina waliowengi wanataka Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina aondolewe madarakani, utawala haramu wa Israel unafanya kila unaloweza kuhakikisha kuwa nafasi ya kiongozi juyo inaimarishwa zaidi na kumfanya aendelee kusalia katika kilele cha uongozi wa Palestina.

Uchunguzi wa maoni uliofanyiwa wakazi 1270 wa Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza kati ya tarehe 15 hadi 18 za mwezi huu wa Septemba, unaonyesha kuwa asilimia 78 ya wakazi wa maeneo hayo wanamtaka Mahmoud Abbas ajiuzulu.

Hii ni katika hali ambayo baraza la mawaziri la utawala ghasibu wa Israel linataka kiongozi huyo kibaraka aendelee kusalia madarakani kwa madhara ya Wapalestina. Tokea serikali mpya ya Wazayuni ichukua hatamu za uongozi katika ardhi unazozikalia kwa mabavu huko Palestina, viongozi wa serikali hiyo wamekuwa wakipaza sauti za kuunga mkono na kutaka Mahmoud Abbas aendelea kuwatawala Wapalestina kinyume na matakwa yao.

Viongozi wa Kizayuni ambao wamekuwa katika mstari wa mbele kuhusu suala hilo ni Benny Gantz, Waziri wa Vita na Isaac Herzog, Rais wa utawala huo ghasibu, ambao wametangaza wazi na rasmi kuwa serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina inapasa kuungwa mkono na kuimarishwa zaidi. Ni kwa kutilia maanani suala hilo ndipo karibuni hivi mkuu wa idara ya usalama ya Israel na kisha wazairi wa vita wa utawala huo wakakutuna na kuzungumza na Mahmoud Abbas kuhusu masuala mbalimbali yanayowahusu Wapalestina na ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu.

Mahmoud Abbas (kushoto) akiwa na Benny Gantz

Swali linaloulizwa hapa ni kuwa je, ni kwa nini Wapalestina wanamtaka Mahmoud Abbas ajiuzulu huku utawala haramu wa Israel ukishikilia kuwa anapaswa kuungwa mkono na kubakishwa madarakani kwa namna yoyote ile?

Tunaweza kutaja sababu mbili katika uwanja huo.

Sababu ya kwanza ni kuwa utendaji wa serikali ya Mahmoud Abbas na serikali yake umewagawanya Wapalestina katika makundi mawili hasimu. Mgawanyiko huo umepelekea taifa la Palestina lisipige hatua yoyote ya maendeleo wala ustawi, bali limekabiliwa na tatizo la kutokuwepo mawasiliano ya dharura kwa ajili ya kujiendeleza. Licha ya kuwa Wapalestina wanasikitishwa na hali hiyo na kutaka kuwepo mfungamano na mshikamano kati yao lakini utawala haramu wa Israel unapinga vikali jambo hilo kwa kuwa linahatarisha maslahi yake haramu katika ardhi unazozikalia kwa mabavu. Kwa hakika utawala wa Israel unataka kuimarisha nafasi ya serikali ya Mahmoud Abbas ili kukabiliana na hatimaye kudhoofisha mapambano ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza. Utawala huo unapanga kutumia vibaya udhaifu uliopatikana ndani ya Palestina kwa madhumuni ya kueneza hitilafu na migawanyiko zaidi kati ya Wapalestina.

Sababu ya pili inahusu mienendo ya kisiasa na kiusalama ya Mahmoud Abbas kuhusiana na Wapalestina na utawala haramu wa Israel. Uamuzi wa Abbas wa kufutilia mbali uchaguzi mkuu wa bunge la Palestina uliokuwa umepangwa kufanyika mwezi Mei uliopita na baada ya kupita miaka 16, uliandamana na ukandamizaji wa polisi dhidi ya wapinzani na waandamanaji waliokuwa wakilalamikia uamuzi huo. Wakati huo huo uchunguzi wa maoni uliofanywa na kituo cha masuala ya usalama kinachofungamana na Chuo Kikuu cha Tel Aviv unaonyesha kuwa wakazi wa Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan wanaamini kuwa tangu achaguliwe kuwa mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina mwaka 2005 Abbas hajafanya lolote la maana na lenye manufaa ya kisiasa kwa ajili ya watu wa Palestina.

Katika hali ambayo Abbas amekataa kushirikiana na makundi ya kisiasa ya Palestina na hasa ya Ukanda wa Gaza, anashirikiana kwa karibu kiusalama na watawala wetenda jinai wa Israel. Kwa sasa Mamlaka ya Ndani ya Palestina inadhamini sehemu kubwa ya mahitaji ya kiusalama ya utawala wa Tel Aviv. Licha ya watawala wa Kizayuni kutekeleza jinai za kutisha dhidi ya Wapalestina na hasa wakazi wa Ukanda wa Gaza lakini bado Mahmoud Abbas na serikali yake ya Mamlaka ya Ndani wameamua kushirikiaka kiusalama na watawala hao na kukataa kukabiliana na askari usalama wa utawala wa Israel wanaoendelea kukanyaga haki na kuwakandamiza Wapalestina bila kujali lolote.

Jinai za Wazayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza

Kwa hakika Mahmoud Abbas anaongoza kundi ambalo linaharamisha kila aina ya mapambano ya silaha dhidi ya Israel na kuona kuwa ushirikiano na Wazayuni dhidi ya maslahi ya Wapalestina na kwa ajili ya kudhibiti hali ya mambo katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni ni jambo la dharura. Ni kutokana na sababu hizo ndipo Wapalestina wakaona udharura wa kujiuzulu Mahmoud Abbas nao utawala haramu wa Israel ukaona udharura wa kubakishwa na kuimarishwa kwake madarakani. Ili kufikiwa lengo hilo la Wazayuni, kituo cha utafiti wa masuala ya kiusalama kinachofungamana na Chuo Kikuu cha Tel Aviv, kinasema kuwa maandamano na malalamiko yaliyofanyika karibuni katika Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan dhidi ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na hasa Mahmoud Abbas mwenyewe yalikuwa hayajawahi kutokea tena huko nyuma na hivyo kuzishauri taasisi za kisiasa na kiusalama za utawala huo zifanye kila linalowezekana kwa ajili ya kuzuia kuondolewa madarakani kiongozi huyo kibaraka.

Tags