Sep 24, 2021 07:43 UTC
  • Meli ya pili ya mafuta kutoka Iran kwa ajili ya Lebanon yatia nanga Baniyas

Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imetangaza kuwa meli kubwa ya pili ya mafuta kutoka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetia nanga katika bandari ya Baniyas nchini Syria.

Taarifa iliyotolewa na Idara ya Mawasiliano ya Umma ya harakati ya Hizbullah ya Lebanon imetangaza kuwa, meli ya pili inayobeba mafuta kutoka Iran ilitia nanga jana saa nne usiku katika bandari ya Baniyas huko Syria. 

Taarifa hiyo imesema kuwa, meli ya kanza ya mafuta kutoka Iran iliwasili kwenye bandari hiyo wiki iliyopita. Shehena hiyo ya mafuta baadaye ilisafirishwa hadi nchini Lebanon.

Mwishoni mwa mwezi uliopita Iran ilikuwa imeionya Marekani isithubutu kuzuia meli zake za mafuta zinazoelekea Lebanon.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alisema Marekani haina haki wala mamlaka ya kuzuia biashara halali baina ya Jamhuri ya Kiislamu na nchi nyinginezo duniani huku akiionya vikali Washington dhidi ya kuzuia meli za mafuta za nchi hii zinazoelekea Lebanon.

Meli kadhaa za mafuta kutoka Iran ziko njiani kelekea Lebanon

Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, viongozi mbalimbali wa Lebanon wakiwemo wa kisiasa na kidini wamekuwa wakisisitiza kuwa, kutumwa meli za mafuta za Iran nchini humo kumewezesha kuvunjwa mzingiro wa Marekani dhidi ya nchi hiyo.

Tangu mwaka uliopita wa 2020 Lebanon imegubikwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi na kisiasa; na katika muda wote huu Marekani imetumia visingizio mbalimbali kuiwekea vikwazo Lebanon na kuwasababishia wananchi wake dhiki na mashaka makubwa ya kimaisha.

Tags