Sep 24, 2021 09:58 UTC
  • Je, kuongezeka ugaidi wa Daesh nchini Iraq ni kujikarabati kundi hilo au ni njama mpya ya Marekani?

Tangu mwanzo wa mwezi huu, magaidi wa Daesh wametekeleza operesheni 16 za ugaidi katika mikoa ya Iraq ya Kirkuk, Swalah ad-Deen na Diyala, ambapo watu zaidi ya 45 wameuawa na kujeruhiwa.

Kuongezeka kwa hasara na maafa yaliyotokana na mshambulio hayo kumepelekea kuibukai mitazamo miwili tofauti kuhusu suala hilo.

Watu wanaoamini kuwa kundi hilo la kigaidi linajaribu kujihuisha na kuchukua sura mpya ya kujikarabati katika ardhi ya Iraq wanasema kuwa kundi hilo limefanya mabadiliko ya msingi katika muundo wake. Moja ya mabadiliko hayo ni kubuni makundi madogo madogo na mengi ambayo hayana mawasiliano makubwa kati yao. Mabadiliko mengine ni makundi hayo kutumia mitandao ya kijamii na hasa ya instagram ili kufikia malengo yao. Mbinu hiyo imewawezesha wanachama wa makundi hayo madogo madogo kuwa na mawasiliano mengi na rahisi miongoni mwao.

Askari vamizi wa Marekani wanatuhumiwa kuimarisha ugaidi wa Daesh Iraq

Mabadiliko hayo bila shaka yamekuwa na natija nzuri kwa magaidi. Moja ya matokeo ya mabadiliko hayo ni kuwawezesha magaidi wa Daesh kujipenyaza zaidi katika jamii ya watu wa Iraq na hivyo kuepuka ugumu wa kuishi kwenye majangwa na milima. Jambo hilo limewafanya wasiweze kutambulika kirahisi na maafisa wa usalama. Mabadiliko hayo pia yamewawezesha Daesh kutekeleza kirahisi operesheni zao za kigaidi kwa kadiri kwamba katika wiki tatu zilizopita wameweza kutekeleza operesheni ambazo zimepelekea Wairaki zaidi ya 45 kupoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa. Hali hiyo imewapelekea baadhi ya Wairaki kuingiwa na wasiwasi mkubwa na kusema  kundi hilo la kigaidi limejikarabati na kudhihiri katika sura mpya.

Mkabala wa mtazamo huo kuna wengine ambao wanaamini kwamba kuongezeka harakati za Daesh nchini Iraq sambamba na kutangazwa mpango wa Marekani wa kuondoa askari wake nchini humo ni njama inayofanywa na nchi hiyo ya Magharibi kwa ajili ya kuhalalisha kuendelea kubaki kwake kijeshi huko Iraq.

Katika uwanja huo, wale wanaopinga kuondoka Marekani wanatumia kisingizio cha kuongezeka ugaidi wa Daesh katika nchi hiyo na kuonya dhidi ya matokeo yake mabaya na kudai kuwa huenda nchi hiyo ikabadilika na kuwa Afghanistan nyingine. Jabbar Yawar, Katibu Mkuu wa Wizara ya Pishmargar ya Kurdistan ambayo ni mmoja wa wapinzani wakuu wa kufukuzwa Marekani kutoka Iraq anadai kwamba Marekani inapasa kubakia daima nchini humo kwa kisingizio kuwa Daesh imezidisha operesheni zake za ugaidi katika nchi hiyo.

Mbali na tahadhari hiyo, kuna wengi ambao wanaamini kuwa hatari ya Daesh Iraq si kubwa kama ilivyokuwa ya Taliban nchini Afghanistan. Kuhusu hilo, Ahmad Abdu as-Sadah, mwandishi wa Kiiraki anasema: "Kinyume na ilivyo Daesh, Taliban ina nafasi kubwa ya kijamii Afghanistan. Kama isingekuwa nafasi hiyo ya kijamii bila shaka kundi la Taliban halingepata fursa nyingine ya kurejea kisiasa Afghanistan na kuteka kirahisi sehemu kubwa ya nchi hiyo. Lakini Iraq, Daesh imepoteza nafasi yake ya kijamii na wala haikubaliki tena katika jamii ya nchi hiyo."

Jinai za Daesh Iraq

Kadhim al-Haj, mtaalamu wa masuala ya kisiasa na kiusalama wa Iraq anasema, kuenezwa hofu na woga kuhusu hatari ya Daesh hakuna ukweli wowote kwa sababu kwanza Daesh haina tena wapiganaji kama ilivyokuwa nao mwaka 2014 na makundi yake yote yamekuwa madogo na yaliyotawanyika sehemu za mbali. Sababu ya pili ni kuwa nguvu ya kijeshi ya Iraq imeimarika na kupata uzoefu mkubwa, na kuwepo nchini makundi tofauti yenye silaha na hasa Hashd as-Sha'bi ni nguvu nyingine inayodhamini usalama wa nchi mkabala wa Daesh.

Nukta ya mwisho ni kuwa huenda operesheni za kigaidi za Daesh zikaongezeka katika kukaribia wakati wa kufanyika uchaguzi wa unge la Iraq na hata katika miezi ya baada ya hapo, yaani wakati wa kukaribia kuondoka askari vamizi wa Marekani katika ardhi ya Iraq, lakini la muhimu hapa ni kuwa hakuna mazingira yoyote yaliyopo ya kubadilika Iraq kuwa Afghanistan ya pili wala kundi la Daesh kubadilika kisiasa na kijamii na kuwa Taliban.

Tags