Sep 26, 2021 11:30 UTC
  • Mahmoud Abbas, rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina
    Mahmoud Abbas, rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina

Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina juzi Ijumaa alisema katika Kikao cha 76 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba wanajeshi wa Israel wamebakiwa na mwaka mmoja wawe wametoka kwenye ardhi za Palestina wanazozikalia kwa mabavu tangu mwaka 1967.

Mahmoud Abbas anayejulikana kwa jina maarufu la Abu Mazen amezungumzia muda huo wa kuendelea wanajeshi wa Israel kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina zilizotekwa mwaka 1967 katika hali ambayo utawala huo katili haujawahi kusita hata siku moja kufanya jinai dhidi ya Wapalestina. Si hayo tu, lakini pia viongozi wa Israel wanaonesha waziwazi na kivitendo kwamba hawashughulishwi na mapatano yoyote yanayofikiwa baina yao na Wapalestina na Waarabu. Hiyo hiyo siku ya Ijumaa ambayo Abu Mazen alitoa matamshi hayo, wanajeshi makatili wa Israel walivamia maeneo tofauti ya Wapalestina huko Nablos, katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kusababisha mapigano baina yao na Wapalestina. Wapalestina 28 walijeruhiwa na mwengine mmoja kuuawa shahidi kwenye jinai hiyo ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni.

Kombora la Qassam la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS

 

Katika hotuba yake kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina alimtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres aitishe kikao kitakachojadili njia za ha kuundwa nchi mbili katika ardhi walizoporwa Wapalestina katika hali ambayo Israel haitambui kabisa uwepo wa nchi inayoitwa Palestina na viongozi wa utawala wa Kizayuni wanasema wazi kuwa kamwe hawawezi kuruhusu kuundwa nchi kama hiyo. Siku moja tu baada ya kurejea kutoka mjini Sharm Sheikh, Misri alikoonana na Rais Abdel Fattah el Sisi wa nchi hiyo, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni, Naftali Bennet alisema hadharani kwamba nchi ya Palestina ni kitu ambacho hakivumiliki na kikubaliki kabisa. Ni kwa sababu hiyo ndio maana wachambuzi wa mambo wakasema kuwa matamshi ya Mahmoud Abbas yamejaa migongano. Kwani kwa upande mmoja anafanya juhudi za kufikia mapatano na viongozi wa utawala wa Kizayuni watenda jinai na katika upande wa pili anataka asipoteze imani ya Wapalestina kwake. Mazungumzo ya hivi karibuni ya Mahmoud Abbas na waziri wa vita wa utawala wa Kizayuni, Benny Gantz yalilalamikiwa vikali na makundi mbalimbali ya Wapalestina ambayo yalitangaza wazi kuwa kufanya mazungumzo na Wazayuni ni kupoteza wakati na kwamba inasikitisha kuona akina Mahmoud Abbas hawapati funzo kutokana na uzoefu mchungu wa huko nyuma.

Hazim Qassim, Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS alisema kuwa mazungumzo baina ya viongozi wa Mamlaka ya ndani ya Palestina na mawaziri na wabunge wa utawala wa Kizayuni kwa ajili ya patano ya pande mbili ni kitu kinachopasa kulaaniwa na hakikubaliki kabisa. Alisisitiza kuwa, mazungumzo hayo yanaonesha jinsi Mamlaka ya Ndani ya Palestina isivyojifunza kutoka kwenye tajiriba chungu za huko nyuma na namna viongozi wa mamlaka hiyo wanavyokwenda kinyume na msimamo wa kitaifa wa Wapalestina.

Ngao ya Chuma ya Israel iliyopewa na Marekani haiwezi kukabiliana na vipigo vya makombora ya Wapalestina

 

Msemaji mwingine wa harakati ya HAMAS, Abdelatif al Qanou alisema kuwa, upatanishi wa Marekani hauna maana yoyote, kwani Washington ni muitifaki mkuu wa utawala wa Kizayuni na haifichi upendeleo wake kwa Israel. Pamoja na hayo, utawala wa Kizayuni hauwezi tena kujidhaminia usalama wake kwani hata "Ngao ya Chuma" imeshindwa kuzuia vipigo vya makombora wanavyopata Wazayuni kutoka kwa wanamapambano wa Kipalestina. Aidha aliitaka Mamlaka ya Ndani ya Palestina isiwe na matumaini hata kidogo na viongozi wa Marekani. 

Kwa kuzingatia yote hayo inaonekana wazi kuwa, matamshi yanayogongana na Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kuhusu matukio ya ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel yanatokana na ahadi chapwa anazopewa na viongozi wa Israel na Marekani ambazo hazina dhamana yoyote ya kutekelezwa.

Kiujumla ni kama yanavyosema makundi ya wanamapambano wa Palestina kwamba njia pekee ya kuweza kukomboa ardhi za Palestina ni muqawama ukiwemo wa silaha kwani hakuna lugha yoyote inayotambuliwa na mabeberu wa dunia zaidi ya mtutu wa bunduki.