Sep 27, 2021 07:31 UTC
  • Jihadul Islami yatoa onyo kali baada ya Israel kuwaua Wapalestina watano

Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina imetoa onyo kali kwa utawala wa Kizayuni wa Israel baada ya utawala huo katili kuwaua shahidi wanamapambano watano wa Palestina.

Katika onyo lake hilo, Jihadul Islami imesema, damu ya Wapalestina waliouawa shahidi katika miji ya Ramallah na Jenin, kwenye Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan hazitaachwa kumwagika vivi hivi bali utawala wa Kizayuni utaonja uchungu wa jinai yake hiyo.

Katika taarifa yake hiyo, Jihadul Islami ya Palesitna pia imesema, jinai za utawala wa Kizayuni zitazidi kuwatia moyo na mori wananchi wa Palestina wa kushikamana zaidi na harakati za muqawama za ukombozi wa taifa lao na watazidi kuona wajibu wa kutumia silaha kupambana na wavamizi wa ardhi zao.

Wanajeshi wa Israel wakiwashambulia kwa risasi wananchi wasio na ulinzi wa Palestina

 

Wanajeshi vamizi wa Israel wamewauwa shahidi kwa kuwapiga risasi wanamapambano watano wa Palestina katika miji ya Jenin na Ramallah kwenye Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Tangu wakati huo, utawala wa Kizayuni umebakia kwenye hofu kubwa ya kulipiziwa kisasi jinai zake hizo.

Alkhamisi iliyopita pia, vyombo vya habari vilitangaza kuuawa shahidi kwa uchache Mpalestina mmoja na kujeruhiwa wengine 28 wakati wanajeshi makatili wa Israel walipovamia maeneo ya Wapalestina huko Nablos na kupambana na wananchi wa maeneo hayo.

Watawala wapya wa Israel wanazidi kuonesha ukatili wao dhidi ya Wapalestina hasa kutokana na Wapalestina hao kuzidi kushikamana na harakati za muqawama.

Tags