Sep 28, 2021 02:25 UTC
  • Ehud Olmert
    Ehud Olmert

Waziri Mkuu wa zamani wa utawala wa Kizayuni wa Israel amekiri kuwa utawala huo haramu hauna uwezo wa kuiua teknolojia ya nyuklia ya Iran.

Ehud Olmert ameeleza hayo katika makala iliyochapishwa na gazeti la Kizayuni la Haaretz na kuongeza kuwa, anakubaliana na makala iliyoandikwa hivi karibuni na Ehud Barak, waziri mkuu mwingine wa zamani wa Israel aliyebainisha kwamba utawala huo wa Kizayuni hauna uwezo wa kuangamiza kile alichokiita "hatari ya nyuklia ya Iran".

Katika makala yake hiyo iliyochapishwa na Haaretz, Olmert amekosoa pia sera za aliyekuwa waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuhusiana na Iran na akasema: kwa kutumia kauli za kichochezi, viongozi wa Israel hawawezi kupata uwezo halisi wa kijeshi wa kuangamiza kikamilifu uwezo wa nyuklia wa Iran kwa sababu mifumo ya operesheni za kijeshi za Israel dhidi ya Iran inahitaji ushirikiano, kujiamini na ustahamilivu wa utawala huo; na muhimu zaidi kuliko yote, ushirikiano wa Marekani.

Kauli hiyo ya waziri mkuu wa zamani wa Israel ya kukiri kwamba utawala huo wa Kizayuni hauna ubavu wa kukabiliana na uwezo wa kinyuklia wa Iran inatolewa katika hali ambayo, kabla yake yeye, makamanda wengi wa kjieshi wa utawala wa Kizayuni walishatamka kuwa jeshi la utawala huo haramu halina uwezo wa kupigana vita vipana na vya kila upande katika eneo.

Kwa mujibu wa makamanda hao wa kijeshi wa utawala wa Kizayuni, ikiwa harakati za Hamas na Jihadul-Islami zimeweza kuiendesha mchakamchaka Israel katika vita vya karibuni vya Ukanda wa Gaza kama ilivyoshuhudiwa, hali itakuwaje ikianzisha vita dhidi ya Hizbullah au Iran?.../

Tags