Sep 28, 2021 02:26 UTC
  • Utawala wa Aal Khalifa umewatesa na kuwasotesha jela mamia ya watoto Bahrain

Vyombo vya habari vimefichua kuwa utawala wa Aal Khalifa umetesa mamia ya watoto nchini Bahrain ili kuwalazimisha wakiri makosa katika jela za utawala huo wa kiimla.

Filamu ya matukio halisi iliyotayarishwa na chaneli ya televisheni ya Aljazeera ya Qatar imefichua kuwa, katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, watoto wapatao 607 wenye umri chini ya miaka 18 wamekumbwa na aina tofauti za mateso ili kulazimishwa kukiri makosa ambayo hawakufanya.

Kwa mujibu wa Aljazeera, nyaraka na ripoti za mashirika ya ndani ya Bahrain na ya kimataifa zinaonyesha kuwa, kuanzia Februari 2011 hadi Agosti 2021, watoto wasiopungua 607 wa Bahrain wamefanyiwa anuai za ukatili, ambapo 259 kati yao wameteswa na wengine 124 wamepuuzwa kupatiwa huduma za tiba wakati wanashikiliwa kwenye jela za utawala wa Manama.

Ripoti ya filamu hiyo ya matukio halisi iliyotayarishwa na Aljazeera imeeleza kuwa, duru kutoka ofisi ya mkuu ya mashtaka zimeieleza televisheni hiyo kwa sharti la kutojitambulisha kuwa, hivi sasa kuna watoto zaidi ya 150 waliowekwa kizuizini kwenye vituo vya jela za utawala wa Aal Khalifa.

Ripoti hiyo imebainisha pia kwamba, kati ya mwaka 2011 na 2021watoto wasiopungua 193 wamehukumiwa kutumikia vifungo jela, huku baadhi yao wakipewa adhabu za vifungo vya maisha.

Bahrain, ambayo idadi kubwa ya wananchi wake ni Waislamu wa madhehebu ya Shia inatawaliwa na utawala wa Kifalme wa aila ya Kisunni ambao umekubuhu katika ukiukaji wa haki za binadamu.

Wafungwa mbalimbali wa kisiasa nchini Bahrain, wakiwemo viongozi wa kidini na wanaharakati

Utawala huo wa kiimla umekuwa ukikandamiza wapinzani tangu ulipotumia mkono wa chuma mwaka 2011 kwa msaada wa Saudi Arabia kupambana na maandamano ya umma ya kupigania mageuzi.

Mbali na adhabu za vifungo, utawala wa Aal Khalifa umewafutia uraia pia mamia ya Wabahrain katika kesi zilizoendeshwa kwa umati na mahakama za utawala huo.

Kwa mujibu wa taasisi za kutetea haki za binadamu, hukumu za adhabu ya kifo zimeongezeka mno pia nchini humo katika muongo mmoja uliopita hasa tangu lilipoanza vuguvugu la Machipuo ya Kiarabu mwaka 2011.../

 

Tags