Oct 01, 2021 02:27 UTC
  • Wabahrain waandamana kupinga waziri wa utawala wa Kizayuni kukanyaga ardhi ya nchi yao

Wananchi wa Bahrain wamefanya maandamano makubwa katika miji kadhaa ya nchi hiyo kupinga waziri wa mambo ya nje wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel kukanyaga ardhi ya nchi yao na kuanzishwa uhusiano wa kawaida na Tel Aviv.

Tovuti ya habari ya Arabi21 imeripoti kuwa, sambamba na waziri wa mambo ya nje wa Israel Yair Lapid kuwasili nchini Bahrain, wananchi wameandamana katika miji mbalimbali kupinga safari ya waziri huyo wa utawala wa Kizayuni katika nchi hiyo.

Mbali na kuchoma moto bendera ya utawala wa Kizayuni na matairi ya magari, waandamanaji hao waliokuwa wamebeba maberamu ya kupinga utawala wa Aal Khalifa walipaza sauti zao pia kutoa nara za kupinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida na Israel.

Watumiaji mitandao ya kijamii nchini Bahrain nao pia wameendesha kampeni maalumu ikiwa na hashtagi za kupinga waziri wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni kuingia katika ardhi ya nchi yao.

Hayo yamejiri, huku ripoti kutoka Bahrain zikieleza kuwa, askari usalama wa utawala wa Aal Khalifa jana Alkhamisi walisambazwa kwenye njia zote zinazoishia uwanja wa ndege wa Manama ili kukabiliana na hatua yoyote iliyohofiwa kuchukuliwa na wapinzani wa utawala huo.

Sheikh Isa Qassim

Wakati huohuo, kiongozi wa Waislamu wa Kishia nchini Bahrain Sheikh Isa Qassim amesema kuhusiana na safari ya waziri wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni nchini humo kwamba, kupatana na adui mzayuni ni vita vya kisiasa vya utawala wa Bahrain dhidi ya watu wa nchi hiyo.

Harakati ya Haq na chama cha Kiislamu cha Al Wifaq nchini Bahrain nazo pia zimesema safari ya Lapid mjini Manama ni utoneshaji wa wazi wa hisia za Wabahrain na kitendo cha uhaini.

Mwezi Septemba mwaka 2020 na kwa upatanishi wa aliyekuwa rais wa wakati huo wa Marekani Donald Trump, Bahrain ilisaini mkataba uliopewa jina la Makubaliano ya Abraham, wa kufanya mapatano na utawala ghasibu wa Israel na kuanzisha rasmi mahusiano ya kidiplomasia na Tel Aviv. 

Hata hivyo wananchi wa Bahrain wametangaza mara kadhaa upinzani wao dhidi ya hatua hiyo ya utawala wa Aal Khalifa.../

 

Tags