Oct 02, 2021 08:13 UTC
  • OIC yalaani uchokozi na uvamizi wa Israel dhidi ya msikiti mtukufu wa Al Aqsa

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC imelaani uvamizi wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel dhidi ya msikiti mtukufu wa Al Aqsa.

Kupitia taarifa iliyotolewa mapema leo, OIC imetahadharisha juu ya matokeo mabaya ya mwendelezo wa sera za utawala wa Kizayuni wa Israel za ujenzi haramu wa vitongoji, uangamizaji kizazi cha Wapalestina, kuwahamisha kwa nguvu wananchi hao madhulumu katika mji wa Baitul Muqaddas (Jerusalem) pamoja na hila zinazoendelea kufanywa na Tel Aviv kwa madhumuni ya kubadilisha hali ya kisheria na kihistoria ya mji huo mtakatifu.

Katika taarifa yake hiyo, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu imelaani pia kitendo cha kupachikwa na kupeperushwa bendera ya utawala ghasibu wa Israel katika msikiti wa Al Aqsa na kuitaka Jamii ya Kimataifa itekeleze wajibu wake na kuulazimisha utawala wa Kizayuni ukomeshe uchokozi na uvamizi wake dhidi ya msikiti huo.

Msikiti wa Al Aqsa ambayo ndiyo nembo kuu ya utambulisho wa Kiislamu na wa Kipalestina katika mji wa Baitul Muqaddas, kila mara umekuwa ukiandamwa na hujuma na hatua haribifu za utawala haramu na dhalimu wa Kizayuni wa Israel.../

Tags