Oct 08, 2021 16:52 UTC
  • Wanamapambano Palestina walaani kuvunjiwa heshima Msikiti wa al Aqsa

Makundi ya mapambano ya ukombozi wa Palestina yametangaza kuwa, kuwaruhusu Wayahudi kufanya ibada katika viwanja vya Msikiti wa al Aqsa ni hatua hatari sana inayovunjia heshima matukufu ya Kiislamu.

Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa na makundi ya mapambano ya ukombozi wa Palestina imesema kuwa, uamuzi uliotolewa majuzi na mahakama ya utawala wa Kizayuni wa Israel unaowaruhusu Wayahudi kufanya ibada katika viwanja vya Msikiti wa al Aqsa ni utangulizi wa kutekeleza njama ya kuugawa msikiti huo baina ya Waislamu na Wayahudi na unawaruhusu walowezi wa Kizayuni kudumisha hujuma na mashambulizi dhidi msikiti huo mtakatifu. 

Taarifa hiyo imesema kuwa, Msikiti wa al Aqsa ni sehemu ya imani na itikadi za Waislamu na kwamba makundi ya mapambano ya Palestina kamwe hayatafumbia jicho hata shibri moja ya ardhi ya Quds na Msikiti wa al Aqsa.

Al Aqsa

Taarifa hiyo imewataka wananchi wote wa Palestina wa Ukingo wa Magharibi na ardhi za Palestina zilizoghusubiwa mwaka 1948 kushiriki kwa wingi katika ibada ya itikafu ndani ya Msikiti wa al Aqsa na kupinga uamuzi wa mahakama hiyo ya Israel. Vilevile imeutaka Umma wa Kiislamu kuitetea Quds na Msikiti wa al Aqsa mbele ya hujuma za Wazayuni na njama zao. 

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) pia Jumatano iliyopita ilitahadharisha kuhusu athari mbaya za uamuzi huo wa utawala wa Kizayuni.   

Tags