Oct 13, 2021 07:39 UTC
  • Israel yaanzisha chokochoko za kijeshi katika miinuko ya Golan ya Syria

Vyombo vya habari vya Kiarabu vimeripoti kuwa, utawala haramu wa Kizayuni wa Israel umeanzisha chokochoko na harakati za kijeshi katika eneo la miinuko ya Golan la ardhi ya Syria.

Televisheni ya Russia al-Yaum imeripoti kuwa, utawala wa Kizayuni umepeleka idadi kubwa ya vifaru kwenye miinuko ya Golan unayoikalia kwa mabavu kwa kutumia malori makubwa.

Hakuna taarifa na maelezo zaidi yaliyotolewa hadi sasa kuhusiana na hatua hiyo ya Tel Aviv.

Harakati na chokochoko hizo zinafanywa katika hali ambayo, katika hatua yenye malengo ya kivamizi na kushadidisha vitendo vya ukatili na utumiaji mabavu, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni Bennett Naftali amesema, miinuko ya Golan ni lengo la kistratejia kwa Israel na kwamba utawala huo haramu umedhamiria kuongeza maradufu idadi ya wakazi wa eneo hilo.

Bennett Naftali

Tangu Syria ilipojipatia uhuru wake, miinuko ya Golan siku zote imebaki kuwa sehemu isiyotenganika na ardhi ya nchi hiyo; na hatua ya utawala ghasibu wa Kizayuni ya kuivamia na kuikalia kwa mabavu miinuko hiyo wakati wa Vita vya Siku Sita vya Juni 1967 kati ya Waarabu na utawala huo, haitabadilisha hali yake ya kihistoria na kisheria.

Ijapokuwa mnamo mwaka 1981 utawala pandikizi wa Israel uliligeuza kisheria eneo la miinuko ya Golan kuwa sehemu ya ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu, lakini jamii ya kimataifa haijawahi katu kuitambua rasmi hatua hiyo na hadi sasa inaendelea kutambua kwamba miinuko ya Golan ni eneo lililovamiwa na linalokaliwa kwa mabavu../.

Tags