Oct 13, 2021 12:55 UTC
  • Hizbullah yaikosoa Marekani kwa kuingilia uchunguzi wa mlipuko wa Bandari ya Beirut

Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imekosoa vikali hatua ya Marekani ya kutia pua katika uchunguzi juu ya mlipuko uliotokea mwaka jana katika Bandari ya Beirut.

Mbunge wa harakati ya Hizbullah, Hassan Fadallah amesema kitendo cha Marekani kujiingiza kwenye uchunguzi huo hakina lengo jingine isipokuwa kutaka kuibebesha dhima kambi hiyo ya muqawama na wapambe wake.

Amesema matamshi ya karibuni ya Washington juu ya uchunguzi huo ni ukiukaji mpya wa mamlaka ya kujitawala Lebanon, na yanalenga kulazimisha uchunguzi huo uendeshwe kwa mujibu wa matakwa batili ya Marekani.

Jana Jumanne, uchunguzi kuhusu mlipuko huo ulisimamishwa kwa muda, kutokana na kile kilichotajwa kuwa changamoto za kisheria zinazozunguka uchunguzi huo unaoendeshwa na Jaji Tarek Bitar.

Kabla ya hapo, Ned Price, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani alidai kuwa, majaji wanaoedesha uchunguzi huo wanatishiwa na mirengo mbalimbali ya Lebanon ikiwemo Hizbullah.

Magofu yaliyosalia baada ya kujiri mlipuko katika Bandari ya Beirut

Hii ni katika hali ambayo, Agosti mwaka huu, Jumuiya ya Mawakili wa Lebanon ilifungua mashtaka katika Mahakama Kuu ya Uingereza mjini London dhidi ya kampuni moja ya nchi hiyo ya Ulaya, kwa tuhuma za kuhusika katika mlipuko huo.

Kampuni hiyo ya Uingereza inatuhumiwa kuhifadhi mamia ya tani za kemikali ya amoniamu naitreti katika Bandari ya Beirut bila ya kuzingatia misingi na kanuni za kisayansi, suala ambalo tarehe 4 Agosti mwaka jana lilisababisha mlipuko huo.

Watu wasiopungua 217 waliuawa katika mlipuko huo na wengine zaidi ya 6,000 walijeruhiwa katika tukio hilo ambalo takwimu zinasema lilisababisha hasara ya zaidi ya dola bilioni 10. 

Tags