Oct 14, 2021 02:19 UTC
  • Vikosi vya ulinzi vya Iraq vyadhibiti kikamilifu eneo la mpaka wa nchi hiyo na Syria

Komandi ya Vikosi vya Gadi ya Mipakani ya Iraq imetangaza kuwa hivi sasa jeshi la nchi hiyo linalidhibiti kikamilifu eneo la mpaka wa Iraq na Syria.

Hamid al Husseini Kamanda wa kikosi cha walinzi wa mpakani cha Iraq ametangaza kuwa, askari jeshi wa ulinzi wa nchi hiyo wameimarisha ulinzi wa maeneo ya mpakani na tayari wamekamilisha kazi ya kuzungushia uzio na ujenzi wa minara katika ukanda wa eneo la mpaka wa nchi hiyo na Syria.  

Taarifa ya kikosi cha ulinzi wa mpakani cha Iraq imeongeza kuwa, walinzi wa mpakani wamechukua hatua kubwa za kudhamini usalama katika mipaka ya Iraq na Syria kuanzia upande wa kaskazini magharibi mwa mkoa wa Nainava na sasa maeneo ya mipakani yako salama. Gadi ya kulinda mipaka ya Iraq pia imefanikiwa kusitisha harakai za magaidi na magendo kupitia maeneo hayo. 

Maeneo ya mpakani kati ya Iraq na Syria ambayo ni jirani na mikoa ya Nainava na al Anbar ni maeneo muhimu sana yanayotumiwa na magaidi kuingia Iraq kutokea Syria. Viongozi wa Iraq wamekiri kuwa, kitendo cha kuziba njia zinazotumiwa na magaidi katika mipaka ya nchi hiyo na Syria kimesaidia sana katika kudhibiti na kufuatilia oparesheni za mamluki wa kundi la Daesh wanaojipenyeza katika maeneo ya magharibi mwa Iraq kutokea Syria. 

Maeneo ya mipaka ya Iraq na Syria 

Iraq imekuwa ikifanya jitihada kubwa za kudumisha amani na usalama katika mipaka yake na Syria tangu baada ya kusambaratishwa kundi la Daesh mwaka 2017. Hata hivyo masalia ya kundi la kigaidi la Daesh wameuwa yakifanya hujuma za kuvizia na za ghafla katika maeneo ya mipaka na kati ya nchi mbili hizo.  

Tags