Oct 14, 2021 13:51 UTC
  • Watu kadhaa wauawa, zaidi ya 60 wajeruhiwa katika mapigano ya silaha mjini Beirut, Lebanon

Duru za habari nchini Lebanon zimeripoti kuwa mapigano makali yanendelea baina ya askari usalama na watu wasiojulikana katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut ambapo idadi ya waliojeruhiwa hadi sasa imepindukia watu 60.

Kwa mujibu wa chaneli ya habari ya LBCI, duru za habari nchini Lebanon zimetangaza kuwa, sauti za milio ya risasi na mifyatuo ya roketi imesikika katika eneo la At-T'ayyunah mjini Beirut ambako mapigano yanaendelea baina ya pande mbili.

Chaneli ya Al Mayadeen imezinakili duru za tiba na kuripoti kuwa idadi ya watu waliofariki imefikia sita na majeruhi wamepindukia watu 60.

Hayo yanajiri huku takwimu za shirika la msalaba mwekundu nchini Lebanon zikionyesha kuwa, watu watano wamefariki na 25 wamejeruhiwa katika mapigano hayo.

Vyombo vya habari vya Lebanon vimeripoti pia kuwa, jeshi la nchi hiyo linaendelea kupeleka askari na zana za kijeshi eneo la mapigano na kwamba magari ya deraya yamesambazwa maeneo ya Ash-Shayah na A'inur-Ramaanah sambamba na kuwaondoa raia katika maeneo hayo.

Mripuko wa bandari ya Beirut

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Lebanon Bassam Mawlawi amesema katika mkutano aliofanya na waandishi wa habari mapema leo kwamba mapigano yalianza baada ya wadunguzi kadhaa kuwafyatulia risasi raia. Mawlawi amesisistiza ulazima wa kuchukuliwa hatua za lazima kulinda harakati za amani za kiraia na kuwatia nguvuni watu wanaobeba silaha.

Mapigano mjini Beirut yalianza baada ya duru za habari za Lebanon kuripoti leo asubuhi kuwa, waungaji mkono wa Hizbullah na harakati ya Amal wamejitokeza mabarabarani kulalamikia utendaji wa Tariq Bitar, mchunguzi mkuu wa faili la mripuko wa bandari ya Beirut.

Muda mfupi baada ya kutangazwa habari hiyo, vyombo vya habari viliripoti kuwa umetokea ufyatuaji risasi zilizolenga raia na kujeruhi watu kadhaa.../

Tags