Oct 15, 2021 02:22 UTC
  • Kuendelea jinai za wanamgambo wa SDF kaskazini mwa Syria kwa uungaji mkono wa Marekani

Kwa mara nyingine tena katika siku za karibuni kumeongezeka jinai zinazofanywa na wanagambo kwa jina la vikosi vya kidemokrasia vya Syria (SDF) dhidi ya wakazi wa maeneo yanayoshikiliwa na wanamgambo hao huko Syria.

Wanamgambo hao ni moja ya makundi yanayopigana katika maeneo ya kaskazini mwa Syria. Wanamgambo hao wanaungwa mkono na kufadhiliwa kwa hali na mali na Marekani na wanaipinga serikali halali ya Syria. Wanamgambo wa SDF wametenda na wanaendelea kufanya jinai chungu nzima dhidi ya raia wa Syria. 

Katika siku za karibuni, wanamgambo hao wa Kikurdi walivamia nyumba kadhaa za wakazi wa kaskazini mwa mkoa wa Deir-Zor kwa msaada wa ndege za wanajeshi vamizi wa Marekani; na kuwapelekea wenyeji kadhaa wa mji huo mahali kusikojulikana. Jumamosi iliyopita pia wanamgambo hao walivivamia vijiji katika kitongoji cha Tell Brak huko kaskazini mashariki mwa al Hasakah na kisha kuwateka nyara raia zaidi ya 100.  

Wanamgambo wa SDF nchini Syria 

Ukweli ni kuwa, mbinu wanayotumia sasa wanamgambo hao ni kuibua hofu na vitisho kwa raia kwa lengo la kuwaibia fedha zao na pia kutaka wawaunge mkono kwa nguvu. Kuhusiana na suala hilo, wanamgambo kwa jina la vikosi vya kidemokrasia vya Syria wametekeleza milipuko kadhaa huko Deir-Zor na huku wakiwa na silaha za kivita wanawalazimisha wenye maduka na wachuuzi wawapatie fedha. 

Huko Hasakah pia wanamgambo wa SDF wanapata pesa kwa kuiba nyaya za umeme na kupora mali za raia majumbani mbali na kuiba vyanzo na maliasili ya nishati katika maeneo ya kaskazini mwa Syria. 

Vitendo hivyo viovu vya wanamgambo hao vimekabiliwa na radiamali ya wananchi. Wakazi wa maeneo yanayodhibitiwa na SDF wamefanya maandamano mara kadhaa kulalamikia jinai na hujuma za wanamgambo hao na kutaka kuzuiwa wanagambo wa SFD kuvamia mali za raia na kutekeleza udhalilishaji mwingine wa kijinsia dhidi ya raia. Amma suala lililo na umuhimu ni kuwa wanamgambo hao kwa jina la vikosi vya kidemokrasia vya Syria wanapewa himaya na kuungwa mkono na Marekani; na ni uungaji mkono huo pia ndio sababu kuu inayowapelekea kuendeleza jinai na machafuko dhidi ya raia katika maeneo mbalimbali wanayoyadhibiti. Marekani kwa upande wake inaendelela kuwaunga mkono wanamgambo hao kwa kisingizio kwamba wanapambana dhidi ya kundi la Daesh, lakini lengo kuu la uungaji mkono wa nchi hiyo kwa  SDF ni kwa ajili ya kuwa na wanamgambo mamluki ambao wataweza kukabiliana na serikali ya Syria.   

Joey Hood Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani alisema Agosti 29 mwaka huu kuwa Daesh bado ni tishio hatari huko Syria na kwamba kundi hilo linastafidi na hali ya mchafukoge nchini humo kutekeleza mashambulizi. Alidai kuwa, Wakurdi wa Syria hawana uwezo wa kuendeleza mchakato wa kupambana na Daesh au kuwalinda maelfu ya wafungwa wa Daesh na familia zao; na kwamba wanajeshi wa Marekani wapo Syria ili kusaidia kutoa pigo na kuliangamiza kundi la Daesh.  

Joey Hood, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani 

Madai hayo yametolewa katika hali ambayo kwa upande mmoja wanajeshi vamizi wa Marekani huko Syria hawapambani na wanamgambo wa Daesh bali zaidi wanachukua hatua ili kuidhoofisha serikali halali ya Damascus; na katika upande mwingine wanamgambo wa Kikurdi si tu hawapigani na Daesh wala magaidi bali rasmi wapo huko kukabiliana na wakazi wa maeneo hayo tajwa ambapo mbali na kupora na kuiba maliasili na vyanzo vya kiuchumi katika maeneo ya kaskazini mwa Syria huiba pia mali za raia wa kawaida.  

Kwa msingi huo, serikali ya Syria imetangaza mara kadhaa kuwa vikosi vya SDF ni vibaraka wa Marekani na Washington si tu inanufaika nao kwa lengo la kukabiliana kijeshi na serikali ya Syria bali inafanya kila iwezalo kuwaunga mkono kwa hali na mali wanamgambo hao ili kuasisi eti eneo linalojitawala la Wakurdi huko kaskazini mwa Syria sambamba na kudhoofisha muundo wa kisiasa wa nchi hiyo na hata kubadili pia  muundo wa jio-politiki wa eneo hilo. 

Marekani ikivilinda vikosi vya SDF vikiiba maliasili ya nishati Syria 

 

Tags