Oct 15, 2021 04:19 UTC
  • Wabahrain waendeleza maandamano ya kupinga uhusiano na Israel

Kwa mara nyingine tena, wananchi wa Bahrain wamefanya maandamano ya kulaani hatua ya utawala wa Aal-Khalifa wa nchi hiyo ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.

Katika maandamano hayo yaliyofanyika katika vijiji vya Sanabis na al-Markh  karibu na mji mkuu Manama, wananchi wa Bahrain wamesema uamuzi huo wa Aal-Khalifa wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Wazayuni unaenda kinyume na matakwa ya Wabahrain walio wengi.

Waandamanaji hao mbali na kutangaza uungaji mkono wao kwa kiongozi wao Sheikh Isa Qassem, wametoa mwito wa kuachiwa huru mara moja wafungwa wa kisiasa wanaoshikiliwa katika mazingira ya kuogofya na vyombo vya usalama vya utawala huo wa kiukoo.

Maandamano dhidi ya utawala wa Kizayuni yalishtadi nchini Bahrain baada ya utawala huo pandikizi kufungua ubalozi wake katika nchi hiyo ya Kiarabu, na vile vile kufuatia safari ya Yair Lapid, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel mjini Manama.

Wabahrain katika maandamano ya kupinga uhusiano na Israel

Miezi michache iliyopita, Bahrain ilitangaza rasmi kufungua ubalozi wake Tel Aviv baada ya pande hizo mbili kufikia mapatano ya kuanzisha uhusiano mwezi Septemba mwaka jana.

Katika dikrii ya Machi 30, Mfalme wa Bahrain, Hamad Bin Isa Aal-Khalifa alitangaza kuanzisha ubalozi wa utawala huo wa kifalme huko Israel na akamteua Khalid Yusuf Al-Jalahma kuwa balozi wake.

Tags