Oct 15, 2021 06:36 UTC
  • Saudia: Tuna nia ya kweli katika mazungumzo yetu na Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia amesema kuwa, nchi yake ina nia ya kweli katika mazungumzo yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Shirika la habari la IRNA limetangaza habari hiyo leo Ijumaa na kumnukuu Faisal bin Farhan Aal Saud akisema hayo katika mahojiano na gazeti la Financial Times na kuongeza kuwa, hadi hivi sasa kumepatikana maendeleo mazuri katika mazungumzo baina ya Tehran na Riyadh.

Vile vile amesema, Saudi Arabia ina hamu ya kuona uhusiano na ushirikiano wa nchi yake na Iran unaimarika katika nyuga zote.

Uhusiano wa nchi mbili za Kiislamu za Iran na Saudia ni muhimu sana katika Ulimwengu wa Kiislamu

 

Kwa mujibu wa gazeti la Financial Times, Saudi Arabia hivi sasa inachunguza ombi la Iran la kufunguliwa tena ubalozi mdogo wa Saudia mjini Mash'had, Iran na ofisi mwakilishi wake katika Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC mjini Jiddah. 

Televisheni ya al Ikhbariya ya serikali ya Saudi Arabia nayo wiki iliyopita ilitangaza kuwa, mazungumzo ya ana kwa ana baina ya Tehran na Riyadh yanaendelea hivi sasa na bila ya shaka mafanikio katika mazungumzo hayo yataleta utulivu na manufaa makubwa kwa eneo hili zima.

Kabla ya hapo pia, Mohammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia alikuwa amesema kwamba, nchi yake inataka kuwa na uhusiano wa kipekee na mzuri na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.