Oct 16, 2021 07:23 UTC
  • Kushindwa Marekani kuzuia kuanzishwa tena uhusiano wa nchi za Kiarabu na Syria

Akizungumza Jumatano mbele ya waandishi habari mjini Washington, Antony Blinken, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amesema nchi hiyo haina nia ya kuunga mkono juhudi za kuboreshwa uhusiano na serikali ya Syria.

Amedai kwamba madamu maendeleo ya kisiasa hayatapatikana huko Syria Marekani haitaunga mkono juhudi za kuimarishwa uhusiano na serikali ya Damascus wala kuondoa vikwazo ilivyowekewa na Washington au kubadilisisha msimamo wake kuhusu ujenzi mpya nchini humo.

Marekani ilikata uhusiano wake wa kidiplomasia na Syria mwaka 2012.

Matamshi hayo ya Blinken yanatolewa katika hali ambayo kinyume na matakwa ya Washington, hata nchi za Kiarabu ambazo zilikuwa zikishirikiana kwa karibu na Marekani katika kutoa mashinikizo ya kuangushwa serikali halali ya Damascus, zote zimebadilisha misimamo yao na sasa ziko mbioni kuhuisha uhusiano wa kisiasa na kiuchumi na serikali ya Rais Bashar al-Asad wa Syria.

Katika uwanja huo, Jordan ambayo ni mmoja wa washirika wakubwa wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi, mwishoni mwa mwezi Septemba alifungua kivuko kikuu cha mpakani kati ya nchi hiyo na Syria ili kuwezesha kufanyika shughuli za kibiashara kati ya nchi mbili. Hatua hiyo ilichukuliwa kuwa dalili muhimu inayothibitisha hamu kubwa zilionayo nchi za Kiarabu kwa ajili ya kuanzisha tena uhusiano na Syria.

Mfalme Abdallah II wa Jordan

Wakati huo huo mwezi huu Mfalme Abdallah II wa Jordan kwa mara ya kwanza katika muongo mmoja uliopita alifanya mazungumzo na Rais Asad katika hali ambayo mawaziri wa mambo ya nje wa Misri na Syria walikutana na kufanya mazungumzo mwezi uliopita pambizoni mwa kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa huko mjini New York. Mazungumzo hayo yalikuwa ya kwanza kuwahi kufanyika katika muongo mmoja uliopita.

Gazeti la Washington Post limechapisha ripoti kadhaa zinazothibitisha kuwa nchi za Kiarabu zimekuwa zikifanya juhudi za kuanzisha tena uhusiano na serikali ya Damascus, jambo ambalo pia limethibitishwa na Rais Joe Biden wa Marekani. Kwa msingi huo matamshi ya karibuni ya Blinken ya kupinga kuboreshwa uhusiano na Syria ni dalili inayothibitisha kwamba kama zilivyokuwa serikali zilizopita za Marekani, serikali ya Biden pia bado inafuatilia juhudi za kutaka kuingusha serikali halali ya Rais Asad wa Syria na kwa hivyo inapinga juhudi zozote za kutambuliwa rasmi au kuimarishwa nafasi ya serikali hiyo.

Pamoja na hayo, lakini serikali za nchi kama vile Imarati na Saudi Arabia ambazo kabla ya hapo zilikuwa katika mrengo mmoja na Marekani katika kujaribu kuiangusha serikali ya Syria sasa zimetambua wazi kwamba siasa na hatua za mrengo wa nchi za Kiarabu na za Magharibi pamoja na Uturuki za kutaka kuiangusha serikali ya Damascus zimegonga mwamba na kushindwa kabisa kufikia lengo lililokusudiwa.

Zimefikia ukweli mchungu kwao kwamba magaidi wote waliokuwa wakitumiwa na kudhaminiwa kwa hali na mali na Marekani na nchi zilizotajwa kwa ajili ya kuiangusha serikali halali ya Syria wote wameshindwa kutekeleza jukumu hilo dhidi ya serikali ya Rais Asad. Sasa mabaki ya magaidi hao walioshindwa na kudhoofishwa kijeshi na serikali ya Damascus yanaoonekana katika baadhi maeneo ya Syria na hasa katika mkoa wa Idlib yakiendelea kupata uungaji mkono wa kifedha na kijeshi kutoka Uturuki na nchi kadhaa za Magharibi.

Tom O'Connor, nchumbuzi wa masual aya kisiasa anasema: Nchi nyingi ambazo zilikata uhusiano na Syria miaka kumi iliyopita sasa zimetambua ukweli mpya wa mambo na kukubali kuendelea kusalia madarakani Rais Asad na hii ni licha ya kuwa Marekani inaendelea kupinga serikali yake.

Rais Bashar Asad wa Syria

Katika uwanja huo, Bahrain na Oman tayari zimefungua balozi zao mjini Damascu na Saudia nayo inaedelea kufanya mazungumzo na serikali ya Syria kwa ajili ya kufungua ubalozi wake mjini humo. Iraq na Lebanon pia zinaendelea kufanya mazungumzo ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na Syria na inatazamiwa kuwa zitafungua balozi zao mjini Damascus hivi karibuni.

Suala muhimu hapa ni kuwa siasa za Rais Joe Biden wa Marekana na hasa za kuharakisha kuondoka askari vamizi wa nchi hiyo huko Afghanistan na kuisaliti serikali ya Kabul, ni jambo ambalo limezithibitishia wazi nchi za Kiarabu na washirika wa Marekani kwamba hakuna dhamana yoyote inayotolewa na nchi hiyo ya Magharibi kwa ajili ya kuzidhaminia usalama wao na kwamba zinapasa kukubali ukweli wa mambo katika eneo, kukiwemo kushindwa siasa zao za uhasama dhidi ya serikali ya Syrian na kuwa sasa zinapasa kuanzisha tena uhusiano na serikali hiyo.

Syria ina umuhimu mkubwa kwa nchi hizo kadiri kwamba haziko tayari tena kuendelea kufuata siasa zilizofeli za Marekani dhidi ya Damascus. Ni wazi kuwa kutofuata nchi za Kiarabu matakwa ya serikali ya Biden ni dalili ya wazi ya kupungua itibari ya Marekani mbele ya waitifaki wake wa eneo la Asia Magharibi.

Tags