Oct 18, 2021 03:51 UTC
  • Vikosi vya Yemen vyatangaza mafanikio mapya Ma'rib na Shabwa

Jeshi la Yemen likishirikiana na vikosi vya kujitolea vya wananchi limepata mafanikio makubwa na kusonga mbele katika mikoa ya Ma'rib na Shabwa kwenye operesheni ya "Machipuo ya Ushindi."

Msemaji wa Jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree alisema hayo jana Jumapili na kuongeza kuwa, muungano wa vikosi vya ulinzi vya Yemen umekomboa miji ya Asilan, Beyhan na Ein mkoani Shabwa, na vile vile miji ya al-Abdiya, al-Harib na sehemu kubwa ya ardhi katika miji ya al-Juba na Jabal Murad katika mkoa wa Ma'rib.

Jenerali Saree amesema muungano huo wa kijeshi wa Yemen kwa ujumla umeshakomboa ardhi yenye ukumbwa wa kilomita mraba 3,200 katika operesheni hiyo ya "Machipuo ya Ushindi." .

Saree ameeeleza bayana kuwa, askari na wapiganaji wa muungano vamizi huko Yemen unaoongozwa na Saudi Arabia wamepata hasara kubwa katika operesheni hiyo.

Jenerali Yahya Saree

Amefafanua kuwa, makamanda wengi wa vikosi vamizi amma wameuawa au kujeruhiwa katika mapigano na jeshi la Yemen likishirikiana na harakati ya kujitolea ya Ansarullah.  

Msemaji wa Jeshi la Yemen ameongeza kuwa, askari na mamluki wengine kadhaa wa wavamizi wametiwa mbaroni katika operesheni hiyo, baadhi yao wakiwa wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS).