Oct 18, 2021 03:51 UTC
  •  Matamshi yanayokinzana ya Rais wa Jamhuri ya Azerbaijan

Wakuu wa serikali ya Jamhuri ya Azerbaijan, hasa Rais wa nchi hiyo Ilham Aliyev, wanaendelea kutoa matamshi yanayokinzana kuhusiana na mapatano na nchi jirani ya Armenia.

Rais wa Jamhuri ya Azerbaijan anaituhumu Armenia kuwa inahusika katika kuuza mihadarati katika nchi za Magharibi wakati ambao, anasisitiza pia kutekelezwa mapatano ya amani baina ya nchi yake na Armenia kuhusu ubadilishanaji mateka chini ya upatanishi wa Russia. Hakuna shaka kuwa,  matamashi yanayokinzana yanatokana na ukosefu wa uweledi katika kiongozi wa kisiasa. Kuhusiana na nukta hii, katika kikao cha Jumuiya ya Madola ya Nchi Huru ambazo ziliwahi kuwa katika Shirikisho la Sovieti (CIS) ambacho kilifanyika Ijumaa huko Minsk, Belarus, Rais wa Jamhuri ya Azerbaijan alisema: "Baku itaikabidhi serikali ya Armenia mateka wote waliokamatwa katika vita vya Nagorno-Karabakh na katika upande wa pili Armenia nayo itakabidhi mateka wa Jamhuri ya Azerbaijan."

Hii ni katika hali ambayo 'Kundi la Minsk' la Shirika la Usalama na Ushirikiano Ulaya barani limezitaka Jamhuri ya Azerbaijan na Armenia zibadilishane mateka wote katika fremu ya mpango unaojulikana kama 'wote mkabala wa wote' na  kwamba zoezi hilo la kuwaachilia huru mateka lifanyike wakati mmoja. Lakini katika kujibu takwa hilo Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Azerbaijan imedai kuwa kila siku Armenia inahataraisha usalama wa raia wake wenye asili ya Azerbaijan na inakataa kutoa ramani kuhusu maeneo yaliko mabomu yaliyotegwa ardhini.

Kwa hakika serikali ya Baku sasa inaweka sharti jipya kwamba, itawaachilia mateka wa Armenia pale tu itakapopewa ramani ya mabomu ya ardhi katika ardhi ya Jamhuri ya Azerbaijan. Hii ni katika hali ambayo sharti kama hilo halikuwepo tokea mwanzo kwani kimsingi hakuna ramani zozote zinazoonyesha maeneo yalikotegwa mabomu ya ardhini na hivyo inaonekana wakuu wa Jamhuri ya Azerbaijan wamekumbwa na tatizo la njama au hitilafu baina yao. 

Kushiriki madola ajinabi katika maamuzi muhimu yanayochukuliwa na serikali ya Jamhuri ya Azerbaijan kumepelekea serikali hiyo ikumbwe na matatizo ambayo yanaendelea kushadidi na kuiweka nchi hiyo katika njia panda. Kuhusiana na nukta hii, Alexander Alezandrian, mtaalamu wa masuala ya Armenia na eneo la Caucasus anasema: "Sera za pamoja za Uturuki na Jamhuri ya Azerbaijan katika kadhia ya Armenia zimegonga mwamba kuhusu udhibiti wa eneo linalozozaniwa la Nagorno-Karabakh. Aidha mgogoro wa Nagorno-Karabakh bado haujatatuliwa na Jamhuri ya Azerbaijan bado haijaweza kudhibiti ukanda wenye ukubwa wa kilomita mraba elfu tatu ambao unakaliwa na watu wenye asili ya Armenia.

Tunapaswa kusema kuwa, matamshi ya Ilham Aliyev yanakuja wakati ambao siku mbili zilizopita aliituhumu Armenia kuwa inahusika na biashara kubwa ya kuuza dawa za kulevya au mihadarati katika nchi za Ulaya kwa kushirikiana na Iran.

Hakuna shaka kuwa matamshi hayo ya Aliyev hayana msingi na yamekanushwa na wakuu wa Iran na Armenia. Madai hayo ya Rais wa Jamhuri ya Azeribaijan yanaonyesha wazi kuwa yeye ni kibaraka wa mabwana zake, yaani utawala wa kibaguzi wa Israel na Marekani na madola mengine ajinabi ambayo yanapinga kuboreshwa uhusiano wa nchi mbili jirani za Iran na Jamhuri ya Azerbaijan. Hivyo Ilham Aliyev yuko tayari kutoa kila aina ya tuhuma na madai bandia kwa ajili ya kuwahudumia na kuwafurahisha mabwana zake Wazayuni na Wamarekani. Ilham Aliyev amekuwa akitoa tuhuma bandia na zilinazokiuka maslahi ya kitaifa ya nchi yake na wakati huo huo siku mbili zilizopita alitaka kuimarishwa uhusiano na Iran. Kwa kuzingatia nukta hiyo, inatubainikia wazi kuwa matamshi yanayotolewa na Ilham Aliyev dhidi ya Iran huwa ni amri kutoka kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kwa maelezo hayo tunaweza kusema kuwa, kwa upande mmoja serikali ya Ilham Aliyev inalazimika kuhudumia madola ajinabi na kutekeleza sera potovu za madola hayo katika eneo la Caucasus na katika upande mwingine inajaribu kuhitimisha mzozo baina yake na Armenia. Matokeo ya kutekeleza sera hizo ni wakuu wa Jamhuri ya Azerbaijan kutoa matamshi  yasiyo sahihi na yanayokinzana mara kwa mara.

Tags