Oct 19, 2021 00:36 UTC
  • Matokeo rasmi ya uchaguzi wa bunge Iraq na mkukuriko wa mirengo ya kisiasa kwa ajili ya kuunda Mrengo Mkuu

Kamisheni Kuu ya Uchaguzi ya Iraq imetangaza matokeo rasmi ya uchaguzi wa tano wa Bunge la nchi hiyo.

Uchaguzi wa mapema wa bunge la tano la Iraq ulifanyika Jumapili ya tarehe 10 Oktoba ambapo asilimia 41 ya watu waliotimiza masharti walijitokeza kupiga kura; na hatimaye baada ya wiki moja, matokeo rasmi ya uchaguzi huo yametolewa.

Hayo yanajiri, wakati matokeo ya awali yalitolewa tarehe 11 Oktoba, siku moja tu baada ya kufanyika uchaguzi huo. Kuchelewa kwa muda wa wiki nzima kutangazwa matokeo rasmi ya uchaguzi wa bunge la Iraq kumetokana na malalamiko ya baadhi ya vyama na makundi kuhusiana na matokeo yaliyotolewa. Kilicholalamikiwa, ni kile kilichotajwa kuwa ni udanganyifu uliofanyika katika uchaguzi. Pamoja na hayo, tukilinganisha malalamiko yaliyotolewa katika uchaguzi wa Oktoba 10 na yale ya uchaguzi wa mwaka 2018, ambapo kulikuwa na makelele mengi ya kulalamikia matokeo, tutabaini kuwa, idadi ya malalamiko rasmi yaliyowasilishwa kwa tume ya uchaguzi kuhusiana na uchaguzi wa Oktoba 10 ni moja tu ya tano, au khumsi ya malalamiko yaliyotolewa katika uchaguzi wa 2018. Kwa maana kwamba, mpaka ulipomalizika muda uliowekwa kisheria kuwasilisha malalamiko, tume ya uchaguzi ya Iraq ilikuwa imepokea malalamiko 356 tu kulinganisha na 1,875 ya uchaguzi wa 2018, ambao haukuwa na makelele mengi ya kulalamikia matokeo.

Wairaqi baada ya kupiga kura katika uchaguzi wa bunge Oktoba 10

Lakini mbali na hayo, hata kama maandamano ya kulalamikia matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 10 yangali yanaendelea katika baadhi ya maeneo ya Iraq, viongozi wa vyama na mirengo ya kisiasa wanaolalamikia matokeo hayo hawatoi kauli za kuchochea vurugu na machafuko ndani ya nchi. Nouri al Maliki, kiongozi wa muungano wa utawala wa sheria, aliyekuwa pia waziri mkuu wa nchi hiyo kwa kipindi cha miaka tisa kuanzia 2005 hadi 2014 ametoa taarifa maalumu, ambayo haikuashiria chochote kuhusu udanganyifu au uchakachuaji wa matokeo ya  uchaguzi, zaidi ya kutoa mwito wa kuondolewa shaka na wasiwasi uliopo juu ya kutolindwa haki za Wairaqi wote. Msimamo huo unaonyesha kuwa, kinyume na baadhi ya chambuzi, Iraq haitatumbukia kwenye lindi la machafuko kwa sababu ya malalamiko ya matokeo ya uchaguzi; na badala yake, makundi ya kisiasa yataingia kwenye awamu nyengine, ambayo ni ya mashauriano ya kuunda Mrengo Mkuu, ambao ndio wenye umuhimu zaidi kwa ajili ya kupendekeza jina la waziri mkuu mpya.  

Suala jengine ni kwamba, baada ya kutangazwa matokeo ya mwisho, imeshafahamika rasmi kuwa muungano wa Saairun unaoongozwa na Muqtada Sadr umewaacha mbali washindani wake kwa kunyakua viti 73, ambavyo ni vingi zaidi mara mbili kulinganisha na viti  37 ulivyopata mrengo wa At-Taqddum unaoongozwa na Muhammad al-Halbousi na viti 34 vilivyonyakuliwa na mrengo wa muungano wa sheria unaoongozwa na Nouri al-Maliki.

Muqtada Sadr

Kulingana na utaratibu rasmi wa kisiasa wa Iraq, waziri mkuu inapasa apendekezwe na mirengo ya Mashia. Kwa hivyo mrengo wa Muqtada Sadr ndio wenye nafasi kubwa ya kuunda Mrengo Mkuu na kupendekeza jina la waziri mkuu. Hata hivyo, ili kuweza kufikia lengo hilo unahitaji viti vingine 92, kwa sababu ili kuwa na Mrengo Mkuu na kuteua waziri mkuu unahitajika uungaji mkono wa asilimia 50 jumlisha na moja ya wabunge, yaani wabunge wasiopungua 165.

Hadi sasa haijafahamika Sadr ataamua kuungana na mirengo gani wakati mashauriano ya kisiasa ya kuunda Mrengo Mkuu yakiwa yameshaanza. Kwa upande wa wapinzani wa muqawama wa Iraq, wao wanafanya juu chini kuhakikisha mrengo huo mkuu unaundwa kwa kuungana mrengo wa Sadr na makundi kama At-Taqaddum na chama cha demokrasia cha Kurdistan na kujumuisha pia makundi madogo madogo na wabunge wa kujitegemea. Wapinzani hao wa muqawama wameweka matumaini maalumu kwa ujumbe uliotolewa na Muqtada Sadr wa kuwa tayari kuzungumza na Marekani huku akitafautiana vikali kimsimamo na Nouri al Maliki na mrengo wa Al-Fat-h.

Pamoja na hayo, ni baada ya kufanyika kikao cha kwanza cha bunge jipya na pengine hata baada ya kutangazwa rais na spika wa bunge ndipo tutaweza kulijadili kwa msisitizo zaidi, suala la Mrengo Mkuu na waziri mkuu mtarajiwa wa Iraq.../ 

Tags