Oct 20, 2021 07:20 UTC
  • Makamanda wanne wa muungano vamizi wa Saudia waangamizwa nchini Yemen

Makamanda wanne wa ngazi za juu wa muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia wameangamizwa katika vita na jeshi na kamati za ukombozi za wananchi wa Yemen.

Shirika la habari la IRNA limevinukuu vyombo vya habari vya muungano vamizi wa Yemen vikitangaza kuwa, Masoud al Sayyad, mkuu wa operesheni wa brigedi ya 143 ya wapiganaji wa nchi kavu wa muungano huo pamoja na Abdul Raqim al Naqash, Ibrahim Ali Naji al Hijri na Wasim Taufiq Ali wameuawa katika vita vinavyoendelea kwenye mkoa wa Ma'rib baina ya muungano huo vamizi na jeshi la Yemen linaloshirikiana na kamati za ukombozi za kujitolea vya wananchi wa nchi hiyo.

Hata hivyo vyombo vya habari vya muungano vamizi wa Yemen havikugusia makamanda hao wanne wa ngazi za juu wa muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia wameuawa wakati gani na mahala gani. Lakini katika siku za hivi karibuni, kumetokea mapigano makali kwenye mkoa wa Ma'rib nchini Yemen huku jeshi la Yemen likiendelea kusonga mbele katika ukombozi wa maeneo yote ya mkoa huo muhimu sana kutoka kwenye makucha ya madola vamizi.

Brigedia Jenerali Yahya Sarii

 

Jumapili wiki hii, Jeshi la Yemen likishirikiana na vikosi vya kujitolea vya wananchi wa nchi hiyo vilitangaza kupata mafanikio makubwa na kusonga mbele katika mikoa ya Ma'rib na Shabwa kwenye operesheni ya "Machipuo ya Ushindi."

Msemaji wa Jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Sarii alisema kuwa, muungano wa vikosi vya ulinzi vya Yemen umekomboa miji ya Asilan, Beyhan na Ein mkoani Shabwa, na vile vile miji ya al-Abdiya, al-Harib na sehemu kubwa ya ardhi katika miji ya al-Juba na Jabal Murad katika mkoa wa Ma'rib.