Oct 20, 2021 07:24 UTC

Wanajeshi makatili wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamevamia sherehe za Maulid ya Mtume Muhammad SAW huko Baitul Muqaddas, Palestina na kujeruhi Waislamu kadhaa.

Shirika la habari la Falastin al Yaum limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, jana Jumanne, wanajeshi wa Israel walivamia sherehe hizo za Maulid ya Mtume Muhammad SAW katika eneo la Bab al Amud, karibu na Kibla cha Kwanza cha Waislamu yaani Msikiti wa al Aqsa, wakawashambulia  kwa risasi Waislamu waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya Maulid na kuwajeruhi kadhaa.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, wanajeshi wa Israel wamewapiga na kuwatolea maneno machafu Waislamu hao wakati wakiwatawanya kwa nguvu na kuvunja Maulid yao. Vijana wasiopungua watano wa Palestina wametekwa nyara na wanajeshi hao makatili wa Israel na kupelekwa kusikojulikana.

Mapenzi makubwa ya Waislamu kwa kiongozi wao, Mtume Muhammad SAW ni ngao kubwa kwao

 

Wanajeshi hao wametumia pia mabomu ya kutoa sauti kali na gesi za kutoa machozi ili kuvunja Maulid ya Waislamu hao wa Palestina.

Jana Jumanne na kwa mujibu wa kalenda ya Palestina, ilisadifiana na mwezi 12 Mfunguo Sita ambayo ni tarehe maarufu zaidi ya siku ya kuzaliwa Bwana Mtume Muhammad SAW kwa Waislamu wa Kisuni.

Kwa vile kuna kauli tofauti kuhusu siku ya kuzaliwa Bwana Mtume Muhammad SAW, huku tarehe maarufu zaidi kwa upande wa Waislamu wa Kisuni ni mwezi 12 Mfunguo Sita na kwa upande wa Waislamu wa Kishia tarehe maarufu zaidi ya kuzaliwa Mtume ni mwezi 17 Mfunguo Sita, Imam Khomeini MA alikitangaza kipindi cha baina ya tarehe hizo mbili kuwa Wiki ya Umoja ili Waislamu waweze kukitumia vizuri kuimarisha umoja na mshikamano baina yao na si kugombana kwa tofauti hiyo ndogo.