Oct 20, 2021 11:38 UTC
  • Sayyid Hassan Nasrullah
    Sayyid Hassan Nasrullah

Hotuba iliyotolewa juzi na Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrullah kuhusu matukio yaliyojiri Alkhamisi iliyopita katika eneo la al Tayune mjini Beirut imetambuliwa kuwa tofauti sana na hotuba zake za miaka ya karibuni.

Alkhamisi iliyopita wafuasi wa Hizbullah na Harakati ya Amal waliomiminika mitaani mjini Beirut kulalamikia utendaji wa jaji Tarek Bitar anayeshughulikia faili la mlipuko wa tarehe 4 Agosti mwaka jana katika Bandari ya Beirut, walishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana ambapo waandamanaji 7 waliuawa na wengine zaidi ya 60 kujeruhiwa. Kabla ya hotuba ya Sayyid Nasrullah, duru za ndani ya Lebanon zilikuwa yatari zimetangaza kuwa, wanamgambo wa kundi linalojiita The Lebanese Forces (LF) linaloongozwa na Samir Geagea ndio waliohusika na jinai hiyo. Vilevile Rais Michel Aoun wa Lebanon amemtahadharisha Geagea kuhusiana na kadhia hiyo.

Katika hotuba yake ya juzi Sayyid Nasrullah, tofauti ya hotuba zake za miaka iliyopita, alililenga moja kwa moja na waziwazi kundi maalumu la kisiasa na kiongozi wake. Alisema: "Chama kimoja hapa nchini kinataka wananchi wakazi jirani na eneo la kusini mwa Beirut waishi kwa waisiwasi, na kinataka kuwadhihirisha Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Lebanon kuwa ni maadui wa Wakristo. Kiongozi wa chama hicho anataka kutengeneza adui bandia wa majirani zetu na lengo wa harakati hiyo ya kuzusha wasiwasi ni kutaka kukidhihirisha chama hicho kuwa ni mtetezi mkuu wa Wakristo. Chama hicho ni The Lebanese Forces (LF)."

Sayyid Hassan Nasrullah

Lengo la Sayyid Hassan Nasrullah kumtaja moja kwa moja Samir Geagea ni kutaka kuzima fitina ya Marekani, Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni wa Israel ambazo zinataka kuitumbukiza Lebanon katika vita vya ndani. Kwa maneno mengine ni kuwa, kwa hotuba yake hiyo ya wazi, Sayyid Nasrullah ameirejesha fitina hiyo inayolenga usalama wa Lebanon na harakati ya Hizbullah kwa kundi hilo hilo la LF. Katika makala yake iliyochapishwa kwenye tovuti ya al Nashrah, mwandishi Mahir al Khatib amesema kuwa: Ujumbe mkubwa zaidi wa hotuba ya Sayyid Hassan Nasrullah ni kutengeneza mlingano wa kiulinzi kwa ajili ya kuzuia vita vya ndani nchini Lebanon."

Nukta nyingine muhimu iliyoashiriwa katika hotuba ya Sayyid Nasrullah ni kwamba Hizbullah haitakubali kuburutwa katika vita vya ndani lakini ina uwezo mkubwa wa kujilinda iwapo maadui wa ndani na nje wataendeleza chokochoko zao. Kuhusu suala hilo Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema: “Hizbullah ina wanajeshi laki moja. Kwa mara ya kwanza tunatangaza waziwazi idadi ya wanajeshi wetu, si kwa shabaha ya kutisha lakini kwa ajili ya kuzuia vita vya ndani.”

Wapiganaji wa Hizbullah

Suala jingine muhimu ni kuwa Sayyid Nasrullah amefanya jitihada za kuwafikishia ujumbe Wakristo wa Lebanon kwamba, Hizbullah haina uadui na Wakristo na kwamba adui halisi wa jamii hiyo ni kundi linalojiita Lebanese Forces (LF).

Akichambua hotuba ya Sayyid Hassan Nasrullah, mwandishi wa Kilebanon Hussein Hardan ameandika: “Miongoni mwa malengo ya jinai iliyofanywa Alkhamisi iliyopita na kundi la Lebanese Forces (LF) katika eneo la al Tayune mjini Beirut ni kutaka kuitumbukiza Hizbullah katika mtego wa fitina na mizozo na hatimaye kuchafua sura na silaha ya harakati hiyo ya mapambano dhidi ya adui mzayuni.”

Katika hotuba yake ya juzi pia Sayyid Nasrullah alifanya jitihada za kuzima vita vya kinafsi vya kundi hilo na kuweka wazi malengo ya fitina zake. Katibu Mkuu wa Hizbullah alisema waziwazi kwamba: “Chama cha Lebanese Forces kimejiunga na Daesh, Jabhatu Nusra na magenge mengine yaliyojiita wapinzani wa Syria; kwa sababu hiyo kinatambuliwa kuwa ni tishio kubwa sana. Hawa ni vibaraka wa Israel. Iwapo Daesh na Jabhatu Nusra wangepata ushindi basi asingesalimika Mkristo hata mmoja. Muungano huu ni tishio kubwa kwa Wakristo wa Syria na Lebanon.”

Tags