Oct 21, 2021 07:18 UTC
  • Hamas: Upanuzi wa vitongoji vya walowezi huko al Aghwar ni tishio kwa Wapalestina

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetangaza kuwa upanuzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika eneo la Palestina la Bonde la Jordan (Aghwar al Urdun) katika Ukingo wa Magharibi ni tishio kwa uwepo wa Wapalestina katika eneo hilo.

Msemaji wa Hamas Hazem Qassim ameeleza kuwa, uamuzi wa utawala wa Kizayuni wa kutaka kupanua vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko al Aghwar una maana ya kuendeleza uvamizi wa utawala huo dhidi ya ardhi na wananchi wa Palestina. Amesema hatua hiyo ya utawala wa Kizayuni wa Israel inalenga uwepo na utambulisho wa Wapalestina. 

Msemaji wa harakati ya Hamas ya Palestina, Hazem Qassim 

Msemaji wa Hamas ameongeza kuwa, mipango ya adui Mzayuni ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi ya Palestina itashindwa na kugonga mwamba kwa mapambano halali ya wananchi wa Palestina ya kuwafurusha Maghasibu katika ardhi hizo. 

Hazem Qassim amesema kuwa, ujenzi wa vitongoji hivyo katika Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan unafanyika huku Mamlaka ya Ndani ya Palestina ikiendelea kuheshimu makubaliano iliyosaini na adui Mzayuni. Amesema, hatua ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina ya kushirikiana na utawala wa Kizayuni katika masuala usalama na pia kukutana na maafisa na mawaziri wa utawala huo ni mwavuli tu wa kufunika sera za ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni za utawala huo.  

Gazeti la Kizayuni la Israel al Yaum jana lilifichua kuwa, Wizara ya Makazi ya utawala huo inajipanga kutekeleza mradi wa kuongeza idadi ya  walowezi wa Kizayuni katika eneo la Palestina la al Aghwar.  

Tags