Oct 22, 2021 03:56 UTC
  • Kuhuishwa uhusiano wa Doha na Cairo katika Muktadha wa Busara ya Qatar katika sera ya kigeni

Kufuatia kuanza kazi kwa balozi wa Qatar mjini Cairo, balozi wa Misri pia aliwasili Doha siku ya Jumatano Oktoba 20 kwa ajili ya kuwakilisha nchi yake katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi.

Tarehe 23 Juni mwaka huu, serikali ya Misri ilimuarifisha Amr Kamal El-Din El-Sherbiny kuwa balozi wake maalumu nchini Qatar. Kabla ya hapo, Salim Mubarakl Aal Shafi, aliwasili mjini Cairo katikati ya mwezi Agosti kwa ajili ya kuanza kazi kama balozi wa Qatar nchini Misri.

Uhusiano wa nchi mbili hizo ulikatwa mwezi Juni 2017. Hiyo haikuwa hatua iliyochukuliwa na Misri pekee bali nchi nyingine tatu za Kiarabu za Saudi Arabia, Bahrain na Imarati zilichukua hatua kama hiyo ili kuishinikiza Qatar na kuifanya isalimu amri mbele ya matwaka ya kidhalimu na kidikteta ya nchi nne hizo. Sababu kuu ya nchi hizo kukata uhusiano wao na Qatar ilitokana na madai ya nchi hizo kuwa serikali ya Doha ilikuwa ikidhamini na kuunga mkono ugaidi, kusudio likiwa ni kundi la Ikhwanul Muslimeen ambalo linatuhumiwa na nchi nne hizo kuwa kundi la kigaidi.

Watawala wa nchi nne za Kiarabu waliokata uhusiano na Qatar

Suala jingine ni kwamba licha ya kuwa uhusiano wa Misri na Qatar ulikatwa mwaka 2017 lakini ni wazi kuwa kabla ya hapo pia yaani tokea mwaka 2013 uhusiano huo haukuwa mzuri. Qatar ilikuwa moja ya nchi zilizounga mkono mwamko na mapambano ya Watu wa Misri dhidi ya utawala wa kidikteta wa Husni Mubarak wa nchi hiyo mwaka 2011 na baada ya hapo pia ikawa miongoni mwa waungaji mkono wakuu wa serikali ya Ikhwanul Muslimeen huko Cairo.

Kwa msingi huo, kuafuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyofanywa dhidi ya serikali ya Ikhwanul Muslimeen iliyokuwa ikiongozwa na Muhammad Mursi mwaka 2013, na kuingia madarakani tena kwa wanajeshi wa Misri uhusiano wa nchi mbili hizo uliharibika pakubwa. Mbali na hayo Qatar ilikuwa miongoni mwa nchi zilizochukulia matukio ya kisiasa Misri mwaka 2013 kuwa mapinduzi ya kijeshi. Licha ya mashinikizo makubwa yaliyotolewa na serikali ya kijeshi ya Abdulfattah as-Sisi dhidi ya Qatar ili ibadilishe msimamo huo lakini viongozi wa Qatar waliendelea kushikilia msimamo wao wa awali kuhusu matukio hayo na wala hawakuwa tayari kulegeza msimamo dhidi ya wanajeshi walioongoza mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Ikhwanul Muslimeen.

Mwenendo wa kuboreshwa uhusiano wa Misri na Qatar ulianza mwanzoni mwa mwaka huu wa 2021. Kabla ya hapo, Saudi Arabia ambayo nayo ilikuwa na uhasama mkubwa na Qatar taratibu ilianza kulegeza msimamo wake dhidi ya nchi hiyo kufuatia mabadiliko ya kiserikali yaliyofanyika Marekani ambapo Joe Biden, ambaye wakati wa kampeni zake za uchaguzi alikosoa vikali siasa za utawala wa kifalme wa Saudia, aliingia madarakani. Januari iliyopita, Qatar ilialikwa kushiriki katika kikao cha Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi kilichofanyika katika mji wa al-Ula nchini Saudi ambapo mapatano ya suluhu yalifikiwa kati ya Qatar na nchi nne za Kiarabu za Saudi Arabia, Misri, Bahrain na Imarati baada ya kupita karibu miaka minne ya kukatwa uhusiano.

Tamim bin Hamad Al Thani wa Qatar

Kuhuishwa uhusiano wa Qatar na Misri kunathibitisha wazi uwepo wa busara katika siasa za kigeni za Doha. Qatar daima imekuwa ikisisitiza umuhimu wa kufanyika mazungumzo baina yake na mahasimu wake na kuchukuliwa hatua za kuondoa mivutano katika uhusiano wa kieneo na kimataifa. Hii ni kutokana na busara ya viongozi wa nchi hiyo wanaomini kuwa ustawi na maendeleo ya nchi yao yanapatikana tu katika utekelezaji wa siasa nzuri za kigeni na zisizo na mivutano.

Kwa msingi huo, mara tu baada ya kuwasili Cairo balozi wa Qatar mwezi Agosti uliopita kwa ajili ya kuanza shughuli zake za kidiplomasia, Jabir al-Harami, mkuu wa vyombo vya habari wa Qatar aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: Uhusiano wa Qatar na Misri umepiga hatua kubwa baada ya mapatano ya al-Ula. Qatar inasisitiza kuwa na uhusiano mzuri wa kigeni na nchi nyingine zikiwemo za Kiarabu na Kiislamu.

 

Tags