Oct 23, 2021 00:19 UTC
  • Kuendelea maandamano ya kulalamikia matokeo ya uchaguzi wa bunge nchini Iraq

Maandamano ya kulalamikia na kupinga matokeo ya uchaguzi wa bunge la Iraq yangali yanaendelea; na sasa yamesambaa hadi mikoa mingine kadhaa ya nchi hiyo.

Uchaguzi wa bunge la Iraq ulifanyika tarehe 10 Oktoba; na matokeo rasmi yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi ya nchi hiyo yanaonyesha kuwa harakati ya Sadr na muungano wa utawala wa sheria unaoongozwa na Nouri al Maliki kwa upande wa mirengo ya Mashia, muungano wa At-Taqaddum wa mrengo wa Masuni unaoongozwa na Muhammad al-Halbousi na chama cha Wakurdi cha demokrasia ya Kurdistan ndiyo makundi yaliyoibuka washindi katika uchaguzi huo.

Kiongozi wa mrengo uliopata viti vingi wa Sadr, Muqtada Sadr 

Pamoja na hayo, matokeo ya uchaguzi huo wa bunge la Iraq yamekabiliwa na malalamiko makubwa. Malalamiko hayo yanashuhudiwa katika sura mbili. Ya kwanza ni ya malalamiko ya makundi ya kisiasa kwa tume ya uchaguzi. Kwa upande huo, tume ya uchaguzi imetangaza katika taarifa kwa vyombo vya habari kuwa, "idadi ya malalamiko ya uchaguzi wa bunge yaliyowasilishwa yamefikia 379 ambapo 361 kati yao yanahusu matokeo ya kura zilizopigwa na wananchi wa kawaida, 27 ya kura zilizopigwa na makundi maalumu na tisa yanahusu zoezi la kuhesabu kura kwa mkono."

Lakini mbali na malalamiko ya vyama na makundi ya kisiasa, wananchi pia wanafanya maandamano kulalamikia matokeo ya uchaguzi wa bunge la Iraq. Mikoa ya Al-Muthanna, Ziqar, Basrah na Baghdad na vilevile miji kadhaa ya katikati na kusini mwa Iraq inashuhudia maandamano ya wananchi. Walalamikaji wanaweka mahema ya kuendesha migomo ya kuketi wakitaka kura zihesabiwe tena. Mjini Baghdad waandamanaji wamepiga kambi na kuweka mahema kandokando ya daraja la mning'inio na karibu la eneo la ulinzi mkali la Green Zone, wakisisitiza kuwa wataendeleza malalamiko yao hadi watakapotekelezewa matakwa yao.

Wairaqi waliopiga kambi wakilaani pia uingiliaji wa Marekani katika uchaguzi

Mlengwa mkuu wa malalamiko hayo ni tume ya uchaguzi. Wananchi na vyama vya siasa nchini Iraq wanaitakidi kuwa kwa upande mmoja, tume hiyo imevurunda sana katika zoezi la kuhesabu kura kwa kufanya uchakachuaji wa kura; na kwa upande mwingine inaendelea kuboronga na kufanya kosa kubwa zaidi kwa kukataa kura zihesabiwe tena kwa mkono.

Wakati huohuo kumekuwepo na ripoti za kupotea kura milioni mbili au kutotolewa vitambulisho karibu milioni moja na laki sita vya kupigia kura, au kuwepo tofauti baina ya idadi ya kura zilizotolewa kwenye vituo vya kupigia kura na zilizotangazwa na tume ya uchaguzi na vilevile kumetolewa madai ya uingiliaji wa nchi za kigeni katika kuzichakachua kura, suala ambalo tume hiyo imelipinga lakini hadi sasa imeshindwa kulitolea majibu ya kukinaisha.

Muhammad Mahdi, mjumbe wa muungano wa Fat-h ana haya ya kunena kuhusiana na suala hilo: "vifaa vya elektroniki vya kuhesabia kura vya tume ya uchaguzi havikuwa na umakini na vimetoa taarifa nyingi zenye makosa. Lakini pamoja na hayo tume ya uchaguzi ingali inapuuza kutafuta njia ya kutatua tatizo hili, na kwa sababu hiyo itabeba dhima ya kuzidi kuwa mbaya inayoshuhudiwa hivi sasa."

Sabah al Ardawi, mwanachama wa harakati iliyoasisiwa karibuni ya "Sheria", yeye pia anasema, tume ya uchaguzi ndiyo inayobeba dhima ya kubadilishwa matokeo ya kura na anasisitiza kwamba, kuna ushahidi wa kuwepo tofauti kubwa ya matokeo ya kura zilizohesabiwa kwa mkono na kwa njia ya elektroniki. Ahmad al-Asadi, msemaji wa muungano wa al-Fat-h, naye pia amesema "tunazo taarifa ambazo zinaonysha kuwa matokeo ya uchaguzi yana walakini."

Waandamanaji katika mji mkuu Baghdad

Baadhi ya wanasiasa nchini Iraq wamethibitisha kuwepo ushawishi na uingiliaji wa Imarati, Uingereza na Marekani katika uchaguzi wa hivi karibuni wa bunge na wanakubaliana na hoja ya uchakachuaji na uingiliaji wa nchi za kigeni katika matokeo ya uchaguzi huo.

Ni kwa msingi huo kamati inayoandaa maandamano ya upinzani ilitangaza siku ya Alkhamisi kuwa, tume ya uchaguzi haifai na ikataka mwenyekiti na wajumbe wengine wa tume hiyo wakabidhiwe kwa vyombo vya sheria na kufunguliwa mashtaka. Kamati hiyo aidha imetaka katika chaguzi zote zitakazokuja kufanyika siku za usoni utumike utaratibu wa kuhesabu kura kwa mkono.../

Tags