Oct 23, 2021 08:12 UTC
  • Haniya: Hatutaghafilika na jukumu tulilonalo la kuwakomboa mateka wa Palestina

Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMS amesisitiza kuwa harakati hiyo haitaghafilika na jukumu ililonalo kuhusiana na mateka Wapalestina.

Ismail Haniya ameyasema hayo akijibu ombi la mbunge wa Jordan Khalil Atiyyah aliyetaka kukombolewa mateka Wajordan wanaoshikiliwa kwenye magereza ya utawala wa Kizayuni wa Israel na akaongeza kwamba, "tutaelekeza juhudi zetu zote katika kuwakomboa mateka Wapalestina na wa Kiarabu, hususan wa Jordan kutoka kwenye jela za ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, na tutalifanikisha hilo kama si leo ni kesho."

Haniya amesema, Hamas haitaruhusu kuwepo masuala ya kimirengo na ya kuwagawa kimakundi mateka wanaoshikiliwa katika jela za Israel, na kwa mara nyingine tena akaitanabahisha jamii ya kimataifa juu ya wajibu ilionao wa kulinda maisha na usalama wa mateka Wapalestina walioko kwenye magereza ya utawala haramu wa Israel.

Mbunge wa Jordan Khalil Atiyyah ameshukuru na kupongeza jithada kubwa zinazofanywa na harakati ya Hamas kwa ajili ya kuwakomboa mateka wanaoshikiliwa kwenye magereza ya Israel na akaiomba tena harakati hiyo iwajumuishe mateka wa Jordan na Wapalestina sita waliotoroka jela ya Israel katika mkataba wa makubaliano ya kubadilishana mateka.

Shirika la magereza ya utawala haramu wa Kizayuni, na hasa baada ya kukimbia mateka sita Wapalestina katika jela moja ya utawala huo dhalimu, limeshadidisha hatua za uvunjaji sheria linazochukua dhidi ya mateka Wapalestina na kutoa adhabu kali za mateso dhidi ya mateka hao.

Takwimu za jumuiya inayoshughulikia masuala ya mateka wa Palestina zinaonyesha kuwa hivi sasa kuna Wapalestina wapatao 4,850, wakiwemo watoto 225 na wanawake 41 wanaoshikiliwa katika magereza ya Israel.../