Oct 24, 2021 04:35 UTC
  • HAMAS yaitaka tena Saudi Arabia iwaachilie huru mahabusu wa Kipalestina

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) kwa mara nyingine tena imeutaka utawala wa Saudi Arabia uwaachilie huru mahabusu wote Wapalestina inaowashikilia na kufunga mafaili yao.

Taarifa ya HAMAS imeashiria ripoti ya Umoja wa Mataifa na kusisitiza kwa mara nyingine tena kuwa, utawala wa Saudi Arabia unapaswa kumuachilia huru Muhammad Saleh al-Khudari, mwanawe na Wapalestina wengine wanaoshikiliwa katika magereza ya utawala huo ambapo wamekuwa wakikumbana na dhulma na ukandamizaji mkubwa.

Mwezi Agosti mwaka huu, Mahakama ya Riyadh iliwahukumu mahabusu 69 wa Palestina na Jordan ambapo aghalabu yao wamehukumiwa kifungo cha miaka 22 jela na wachache walioasalia kifungo cha miezi sita jela. Mahakama hiyo aidha ilimruhusu mtu mmoja tu wa familia ya kila mfungwa kuhudhuria kikao cha kesi hizo.

Nembo ya harakati ya Hamas

Watawala wa Saudi Arabia na licha ya matakwa ya kila mara ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS), asasi za haki za binaadamu na familia za watu wanaoshikiliwa huko Saudia, bado wamekataa kuwaachilia huru Wapalestina hao.

Tangu mwaka juzi, (2019) Saudi Arabia imewatia mbaroni zaidi ya Wapalestina na Wajordan 60 kwa tuhuma zinazohusiana na kuwa wanachama wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS).

Utawala vamizi wa Saudia ambao umeendelea kufanya mauaji dhidi ya wananchi wasio na hatia wa Yemen umekuwa ukiandamwa na ukosoaji mkubwa wa mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binadamu kutokana na kukiuka haki za binadamu nje na ndani ya nchi hiyo ya Kiarabu.

Tags