Oct 24, 2021 15:14 UTC
  • Hizbullah: Tutawaadhibu waliohusika na ghasia za umwagaji damu Beirut

Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amemkosoa vikali Jaji Tarek Bitar anayeongoza uchunguzi wa mlipuko uliotokea mwaka jana katika Bandari ya Beirut na kusisitiza kuwa, hakimu huyo anapaswa kutimuliwa kwa kuwa anaingiza siasa kwenye kadhia hiyo.

Sheikh Naim Qassem alisema hayo jana jioni mjini Beirut na kueleza bayana kuwa, watu waliohusika na ghasia za umwagaji damu mjini Beirut siku chache zilizopita wataadhibiwa kwa mujibu wa sheria.

Alkhamisi ya wiki iliyopita, wafuasi wa Hizbullah na Harakati ya Amal waliomiminika mitaani mjini Beirut kulalamikia utendaji wa jaji Tarek Bitar anayeshughulikia faili la mlipuko wa tarehe 4 Agosti mwaka jana katika Bandari ya Beirut, walishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana ambapo waandamanaji 7 waliuawa na wengine zaidi ya 60 kujeruhiwa.

Wanamgambo wa kundi linalojiita The Lebanese Forces (LF) linaloongozwa na Samir Geagea ndio waliohusika na jinai hiyo mjini Beirut. 

Wanamgambo wa LF wakiwafyatulia risasi waandamanaji mjini Beirut

Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amebainisha kuwa, wanamgambo wa Lebanese Forces wakishirikiana na mamluki wa kigeni walitanguliza mbele maslahi yao katika fujo hizo, pasi na kujali hali mbaya ya kiuchumi na kijamii inayowasumbua wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu. 

Aidha mwanachuoni huyo wa Kiislamu nchini Lebanon amesema Jaji Bitar anapaswa kubebeshwa dhima kwa vitendo vya uhaini vilivyofanyika katika maandamano ya amani yaliyofanyika katika eneo la Tayyoune mjini Beirut.

 

Tags