Oct 25, 2021 02:34 UTC
  • Hivi ndivyo majeshi ya Yemen yalivyoendesha operesheni ya ukombozi wa kilomia 3200

Msemaji wa vikosi vya ulinzi vya Yemen ametoa ufafanuzi kuhusu operesheni ya "Machipuo ya Ushindi" katika mikoa ya Shabwa na Ma'rib iliyofanikisha kukombolewa kilomita 3200 za ardhi ya Yemen.

Brigedia Jenerali Yahya Saree ambaye Jumapili ya tarehe 17 Oktoba alitangaza habari ya kufanyika kwa mafanikio makubwa operesheni ya "Machipuo ya Ushindi" katika mikoa hiyo miwili iliyokuwa imetekwa kikamilifu na wanajeshi vamizi wanaoongozwa na Saudi Arabia, jana Jumapili tarehe 24 Oktoba alitoa ufafanuzi juu ya jinsi operesheni hiyo ilivyofanyika.

Amesema, katika operesheni hiyo ya kishujaa, jeshi la Yemen kwa kushirikiana na kamati za kujitolea za wananchi wa nchi hiyo lilifanya zaidi ya operesheni 287 ambazo ni pamoja na operesheni 161 za ndani ya ardhi ya Yemen na 117 za ndani ya ardhi ya nchi vamizi ya Saudi Arabia.

Brigedia Jenerali Yahya Saree akitoa ufafanuzi jinsi operesheni ilivyofanikishwa

 

Msemaji huyo wa majeshi ya Yemen pia amesema, operesheni hizo zimefanyika katika wilaya za Asailan, Bihan na Ain mkoa Shabwa na katika wilaya za Harib na al Abadiyyah na eneo kubwa la wilaya za Jabal Murad na al Juba mkoani Ma'rib na kiujumla kufanikiwa kukomboa kilomia 3200 za mikoa hiyo miwli kutoka katika makucha ya muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia.

Siku chache zilizopita pia, kuliripotiwa kuwa, makamanda wanne wa ngazi za juu wa muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia wameangamizwa katika vita na jeshi na kamati za ukombozi za wananchi wa Yemen. Vyombo vya habari vya muungano vamizi wa Yemen vilitangaza kuwa, Masoud al Sayyad, mkuu wa operesheni wa brigedi ya 143 ya wapiganaji wa nchi kavu wa muungano huo pamoja na Abdul Raqim al Naqash, Ibrahim Ali Naji al Hijri na Wasim Taufiq Ali wameuawa katika vita vya mkoa wa Ma'rib.