Oct 25, 2021 11:17 UTC
  • Ndege ya kwanza ya moja kwa moja kutoka Saudia kutua Israel

Kwa mara ya kwanza, ndege ya moja kwa moja kutoka Saudi Arabia inatazamiwa kutua usiku huu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kwa mujibu wa shirika la habari la KAN, ndege hiyo ya shirika la Imirati la Royal Jet itatua usiku huu katika Uwanja wa Ndege wa Ben-Gurion ikitokea Riyadh, katika hatua ambayo kwa mara nyingine tena inadhihirisha jitihada za utawala wa Aal-Saud na utawala wa Kizayuni wa Israel za kuimarisha uhusiano wa pande mbili.

Haya yanajiri baada ya Jake Sullivan, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Ikulu ya White House ya Marekani kumshinikiza Muhammad bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia kuanzisha uhusiano wa kawaida na Tel Aviv.

Ikumbukwe kuwa, mwaka 2018, Saudi Arabia ilifungua anga yake kwa mara ya kwanza na kuziruhusu ndege za shirika la Air India kutumia anga hiyo katika safari zake za kwenda na kutoka Israel.

Uwanja wa Ndege wa Ben-Gurion 

Kabla ya hapo, Muhammad bin Salman alifanya safari za siri huko Israel ambapo alikutana na viongozi wa ngazi za juu wa utawala huo haramu unaozikalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina.

Wadadisi wa mambo wanasema hatua hizi za Riyadh zinalenga kuandaa mazingira ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel, ikifuata mkumbo wa Imarati, Bahrain, Morocco na Sudan.

Tags