Oct 26, 2021 08:00 UTC
  • Wanawake 33 wa Kipalestina wanazuiliwa katika mazingira ya kutisha Israel

Shirika moja huru la kutetea haki za binadamu limesema makumi ya wanawake wa Palestina wanashikiliwa katika mazingira ya kuogofya na yasiyo ya kibinadamu na vyombo vya usalama vya utawala wa Kizayuni wa Israel katika gereza la Damon.

Taarifa ya Kituo cha Mafunzo ya Wafungwa wa Palestina (PCBS) imebainisha kuwa, wanawake 33 wa Kipalestina wakiwemo maajuza kadhaa wanaosumbuliwa na matatizo ya kiafya wanapitia kipindi kigumu katika gereza hilo la kutisha la Wazayuni.

Kituo hicho kimeonya kuwa, Idara ya Magereza ya Israel imeshadidisha mbinu za mateso na ukandamizaji dhidi ya wafungwa hao wanawake wa Kipalestina, ikiwemo kuwanyima matibabu kwa makusudi na kuwapiga faini eti kwa kukiuka kanuni za jela.

Jumuiya ya Mateka na Wafungwa wa Palestina ilitangaza hivi karibuni kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel umewatia nguvuni zaidi ya Wapalestina milioni moja tangu mwaka 1967.

Gereza la Ofer la Israel

Kwa mujibu wa jumuiya hiyo, elfu 50 kati ya Wapalestina hao waliokamatwa na utawala haramu wa Israel walikuwa watoto, na zaidi na elfu 17 miongoni mwao ni wanawake.

Kwa sasa zaidi ya Wapalestina elfu nne na mia nane wakiwemo watoto na wanawake wanashikiliwa katika jela na korokoro za kutisha za Israel ambako wanakabiliana na sulubu na mateso makubwa. 

Tags