Oct 26, 2021 08:06 UTC
  • Jasusi wa zamani wa Saudia: Bin Salman ni katili, ana matatizo ya kiakili

Afisa wa zamani wa Idara ya Ujasusi wa Saudi Arabia amemtaja Mohammad bin Salman, mrithi wa ufalme wa Saudia kama mtu katili, asiye na chembe ya utu na mwenye matatizo ya kisaikolojia.

Saad Aljabri ambaye pia amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Saudia, Mkuu wa Idara ya Intelijensia na mshauri mkubwa wa aliyekuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia,  Mohammed bin Nayef amesema hayo katika kipindi cha mahojiano cha "60 Minutes" cha kanali ya televisheni ya CBS.

Aljabri ambaye anaishi uhamishoni nchini Canada tokea mwaka 2017 baada ya Bin Salman kutwaa nafasi ya mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia kutoka kwa Bin Nayef amesema mrithi huyo wa ufalme wa Saudia anapanga njama za kumuua, kwa kuwa anajua siri zake nyingi na za ukoo unaotawala Saudia wa Aal-Saud. 

Mkuu huyo wa zamani wa ujasusi wa Saudia amesema, "Nipo hapa kupiga kengele ya hatari kuhusu mtu mwenye matatizo ya kiakili na muuaji katika eneo la Mashariki ya Kati, mwenye rasimali chungu nzima, na ambaye ni tishio si tu kwa watu wake (Wasaudia) bali kwa Wamarekani na sayari ya dunia kwa ujumla."

Mwandishi wa habari Jamal Khashoggi aliyeuawa na maajenti wa Saudi Arabia huko Uturuki 

Aljabri ameeleza bayana kuwa, " Bin Salman hana hisia za kibinadamu, hajifunzi kutokana na makosa yake, na tumeshuhudia jinai na uhaini uliofanywa na katili huyu."

Mwaka jana, Aljabri aliwasilisha mashtaka katika mahakama moja ya Marekani akisema kuwa, Muhammad bin Salman mwaka 2018 alituma timu ya kumuua yeye, ingawa njama za mauaji hayo zilisambaratishwa na viongozi wa Canada.