Oct 26, 2021 12:17 UTC
  • Umoja wa Mataifa wataka kufunguliwa vivuko vya Ghaza huko Palestina

Umoja wa Mataifa umeutaka utawala wa Kizayuni wa Israel uheshimu sheria za kimataifa na uache kuuzingira Ukanda wa Ghaza. Umoja huo umeitaka Israel ifungue vivuko vyote vya kuingia na kutoka katika ukanda huo.

Shirika la habari la FARS limemnukuu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres akitoa mwito huo kwenye ripoti yake ya kila mwaka kwa Baraza Kuu la umoja huo na kulalamikia vitendo vya kiuadui vinavyofanywa na Wazayuni dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Palestina.

Katika ripoti yake hiyo, Guterres ameitaka Israel iache kufunga vivuko vya Ukanda wa Ghaza na iruhusu wakazi wa eneo hilo waishi kwa uhuru na waweze kuingia na kutoka katika ukanda huo bila ya kizuizi chochote. Ukanda wa Ghaza unahesabiwa kuwa ni jela kubwa zaidi ya binadamu duniani hivi sasa kutokana na utawala wa Kizayuni kufunga njia zote za kuingia na kutoka katika eneo hilo, angani, majini na ardhini kwa miaka mingi sasa.

Israel inafanya jinai kubwa dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Ghaza huko Palestina

 

Utawala wa Kizayuni ulianza kuuzingira kila upande Ukanda wa Ghaza mwaka 2006 baada ya wananchi wa Palestina kutumia haki yao ya kidemokrasia ya kuichagua Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS kuwaongoza.

Si hayo tu, lakini pia utawala wa Kizayuni umekuwa ukifanya mashambulio ya mara kwa mara dhidi ya wakazi wasio na hatia wa ukanda huo ikiwa ni pamoja na kuendesha vita vikubwa vya kikatili kwa kutumia silaha zilizopigwa marufuku dhidi ya Wapalestina wa eneo hilo.