Oct 27, 2021 04:05 UTC
  • Kuendelea kupuuza Israel upinzani wa walimwengu kwa ujenzi wa vitongoji vya walowez wa Kizayuni

Uamuzi wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel wa kujenga nyumba nyingine mpya katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan umekabiliwa na upinzani mkali wa Umoja wa Ulaya na baadhi ya mataifa katika eneo la Asia Magharibi.

Katika hatua yake mpya, Israel imeamuua kujenga nyumba mpya 1,355 kwa ajili ya walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan unaokaliwa kwa mabavu. Waziri wa Nyumba wa utawala vamizi wa Israel ametangaza kuwa, kujengwa nyumba mpya huko Judea na Samaria ni sehemu mipango ya uwekezaji ya utawala huo.

Ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika maeneo ya Wapalestina ni miongoni mwa siasa thabiti na za kuendelea za utawala haramu wa Israel ambapo hakuna Waziri Mkuu yeyote wa utawala huo aliyewahi kushika wadhifa huo na akasitisha mpango huo katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu; bali kila aliyeingia madarakani aliliendeleza hilo kwa nguvu zake zote. Kuna sababu kuu kadhaa ambazo ni muhimu kwa Wazayuni kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi.

Moja ya sababu hizo ni kuwa, ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi unafanyika kwa shabaha ya kusukuma mbele gurudumu la kupanua ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Israel.

Ujenzi wa Vitongoji vya walowezi wa Kizayuni unakwenda sambamba na kubomoa nyumba za Wapalestina

 

Kupanuliwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kuna uhusiano wa moja kwa moja na falsafa ya uwepo wa utawala huo bandia. Kwa kukalia kwa mabavu zaidi ya aslimiam 85, utawala huo kimsingi umepora ramani na jiografia ya Palestina na kuunganisha na ardhi ulizozikalia kwa mabavu mwaka 1948. Hata hivyo hatupaswi kusahau kwamba, hayo yote yanatimia kwa himaya na uungaji mkono wa madola makubwa na ya kibeberu duniani hususan Marekani.

Sababu ya pili muhimu ya sisitizo la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel la kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni ni kwamba, utawala huo unakabiliwa na mgogoro wa idadi ya watu. Idadi ya Mayahudi ambao wanaingia Israel kutoka katika mataifa mengine wamekuwa wakiahadiwa mambo mengi ambapo moja ya ahadi hizo ni kwamba, wasiwe na wasi wasi kuhusiana na suala la uchumi hususan nyumba na makazi. Kwa muktadha huo, Israel kwa kujenga nyumba mpya inafanya juhudi za kuzuia Mayahudi waliowasili huko kwa ahadi ya kupata nyumba wasije wakabadilisha uamuzi na kuamua kurejea walikotoka. Ili kujenga nyumba mpya 1,355, utawala dhalimu wa Israel utalazimika kutoa dola milioni 70 kwa ajili ya kugharimia ujenzi huo.

Jambo jingine ni kuwa, baraza la sasa la mawaziri la Israel limechukua uamuzi wa kujenga vitongoji vipya vya walowezi wa Kizayuni katika hali ambayo, Naftali Bennett, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel ametangaza mara kadhaa kwamba, haungi mkono suala la kuundwa madola mawili kwa ajili ya kuupatia ufumbuzi mzozo wa Palestina na Israel, lakini hataendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi.

Naftali Bennett, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel

 

Kwa msingi huo, uamuzi wa hivi karibuni wa Israel wa kujenga nyumba mpya kwa ajili ya walowezi wa Kizayuni unaonyesha kuwa,  Bennett ameamua kutekeleza mpango huo na kupuuza sheria za kimataifa ili kutafuta himaya na uungaji mkono wa Wazayuni.

Desemba 2016 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio 2334 ambalo liliutaka utawala haramu wa Israel usimamishe haraka na kikamilifu shughuli zote za ujenzi wa vitongoji katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu. Hata hivyo Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa zamani wa Israel akipata himaya na uungaji mkono wa aliyekuwa Rais wa Marekani Donald Trump alipuuza azimio hilo. Filihali Naftali Bennett naye amefuata mkondo huo huo wa kupuuza azimio hilo la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Nukta nyingine ni kuwa, uamuzi wa Waziri Mkuu Naftali Bennett wa kujenga nyumba nyingine mpya za walowezi wa Kizayuni umekabiliwa na upinzani mkali wa jamii ya kimataifa na eti Marekani nayo imeonyersha wasiwasi kwa hatua hiyo.

Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya

 

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani ameonyesha wasiwasi alionao kwa hatua hiyo ya Israel. Nayo ofisi ya Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya imetoa taarifa na kutoa wito wa kusitishwa mpango huo. Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni unaofanywa na Israel ni hatua iliyo inyume na sheria na kwamba, vitongoji hivyo ni kizingiti cha kufikiwa amani ya kudumu na ya pande zote. Serikali ya Misri nayo imetoa taarifa na kupinga uamuzi huo wa Tel Aviv.

Licha ya upinzani wote huo, lakini utawala huo ghasibu umetia pamba masikioni na kuendelea kukiuka haki za Wapalestina. Kimsingi ni kuwa, utawala ghasibu wa Israel umefikia natija hii kwamba, upinzani wa jamii ya kimataifa ni sawa kelele tu chura ambazo hazimzuii ng'ombe kunywa maji.