Oct 27, 2021 13:01 UTC
  • Kundi la kigaidi la DAESH laua raia wengine kadhaa wasio na ulinzi wa Iraq mkoani Diyala

Duru za usalama za Iraq zimetangaza kuwa, magaidi wa kundi la ukufurishaji la DAESH (ISIS) wameshambulio kijiji kimoja mkoani Diala na kuwaua na kuwajeruhi raia kadhaa wasio na ulinzi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na duru hizo leo, magaidi wa kundi la Daesh wameua raia wasiopungua saba katika shambulio dhidi ya kijiji cha al Amam kilichoko karibu na kijiji cha al-Hawasha kilichoshambuliwa usiku wa kuamkia leo.

Kwa mujibu wa duru hizo za usalama, katika shambulio hilo, magaidi hao walichoma moto pia konde za wanakijiji hao na kuiba magari kadhaa.

Hayo yanajiri wakati Kamandi ya Operesheni ya Pamoja ya vikosi vya Iraq ilitangaza mapema kuwa, watu wapatao 33 waliuawa na kujeruhiwa katika shambulio la kigaidi lililolenga kijiji cha al-Hawasha usiku wa kuamkia leo, karibu na mji wa Muqdadiya, mkoani Diyala mashariki mwa nchi hiyo.

Polisi ya Iraq imesema, magaidi wa kundi la Daesh walitumia magari kadhaa na bunduki katika shambulio hilo.

Maafa wa shambulio la kigaidi nchini Iraq

Maafisa katika eneo hilo wamesema, awali magaidi hao waliwateka nyara wanakijiji wawili na baadaye wakakishambulia kijiji hicho baada ya kutotekelezwa takwa lao la kulipwa kikomboleo. Imeelezwa kuwa watu wote waliouliwa na kujeruhiwa walikuwa raia.

Wakati huohuo, Rais Barham Salih wa Iraq amelaani mauaji hayo ya kigaidi ambayo amesema yanalenga kuvuruga uthabiti na utulivu nchini humo.

Katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa twitter, Salih amesema Iraq inahitaji kuimarisha usalama wake, kushughulikia nyufa za kiusalama na kutodharau kitisho cha kundi la Daesh.

Tangu liliposambaratishwa nchini Iraq mnamo mwaka 2017 kundi la kigaidi na ukufurishaji la DAESH (ISIS) limekuwa likifanya hujuma na mashambulio ya kuvizia.

Ripoti iliyotolewa mapema mwaka huu na Umoja wa Mataifa imekadiria kuwa, kuna magaidi wapatao 10,000 waliosalia wa kundi hilo, wanaoendeleza hujuma zao katika nchi mbili za Iraq na Syria, zikilenga pia vikosi vya usalama, vituo vya umeme na miundomsingi mingine.

Watu wasiopungua 30 waliuawa na makumi ya wengine walijeruhiwa mnamo mwezi Julai wakati bomu lililotegwa kando ya barabara liliporipuka kwenye kiunga cha mji mkuu Baghdad katika soko lililokuwa limefurika watu.

Mwezi Januari pia, mabomu pacha yaliyoripuliwa na magaidi waliojitoa mhanga wa kundi la Daesh yaliua watu 32 na kujeruhi makumi ya wengine katika soko lililokuwa limejaa watu katika mji mkuu huohuo wa Iraq.../ 

Tags